1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shirika la WHO latuliza hofu ya aina mpya ya virusi

Yusra Buwayhid
22 Desemba 2020

Shrika la Afya Duniani WHO limetahadharisha dhidi ya wasiwasi wa kupindukia kuhusu aina mpya ya virusi vya corona vinavyosamba kwa kasi kubwa, baada ya kugunduliwa nchini Uingereza na baadae Afrika Kusini.

https://p.dw.com/p/3n20M
Südafrika Corona-Pandemie Soweto Test
Picha: Jerome Delay/AP Photo/picture alliance

Shirika hilo la WHO limesema ni kawaida ya virusi kufanya hivyo wakati wa janga, baada ya aina hiyo ya virusi kuzua taharuki kote ulimwenguni, hali iliyopelekea mataifa kadhaa kuweka vizuizi vya usafiri kwa Uingereza na Afrika Kusini.

Soma zaidi: Ubelgiji na Uholanzi zapiga marufuku ndege kutoka Uingereza

Maafisa wa WHO wamesema hawana ushahidi wowote unaoonyesha kwamba aina hiyo mpya ya virusi inawafanya watu kuwa wagonjwa zaidi au kuwa ni mbaya zaidi kuliko virusi vilivyokuwepo awali vya ugonjwa wa  COVID-19. Ingawa WHO imethibitisha kwamba aina hiyo mpya inaonekana kuenea kwa kasi zaidi.

"Kufikia sasa, ingawa tumeona mabadiliko kadhaa katika virusi vya corona, hakuna hata aina moja iliyoleta athari yoyote katika tiba zinazotumiwa kwa sasa, dawa au chanjo inayoendelea kufanyiwa uchunguzi na matumaini yetu ni kwamba hali hii itaendelea kuwa hivyo," amesema Mwanasayansi Mkuu wa WHO, Soumya Swaminathan katika mkutano wa njia ya video huko Geneva.

Kulingana na WHO, chanjo zilizotengenezwa kupambana na COVID-19 zina uwezo wa kutoa kinga dhidi ya aina hiyo mpya ya virusi vya corona. Lakini uchunguzi zaidi unaendelea kufanywa na wanasayansi.

Umoja wa Ulaya waidhinisha mauzo ya chanjo BioNTech-Pfizer

Wakati hayo yakijiri, Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya imeidhinisha kwa masharti mauzo ya chanjo iliyotengenezwa na kampuni ya Pfizer ya Marekani kwa ushirikiano na kampuni ya Ujerumani BioNTech.

USA Biden lässt sich gegen COVID impfen
Rais mteule wa Marekani Joe Biden, akidungwa sindano ya chanjoPicha: Alex Edelman/AFP

Rais wa halmashauri hiyo, Ursula von der Leyen, amesema akiwa mjini Brussels kwamba hii ni hatua muhimu katika juhudi za kuutafutia dawa ugonjwa wa COVID-19.

Ni chanjo ya kwanza dhidi ya virusi vya corona kuidhinishwa na Umoja wa Ulaya. Na itaanza kutolewa katika mataifa tofauti ya Ulaya mwezi huu. Hapa nchini Ujerumani, wanachi wataanza kudungwa chanjo hiyo mnamo Decemba 27.

Wafanyakazi wa huduma za afya na watu wengine walio katika hatari kubwa, tayari walianza kupewa chanjo hiyo ya BioNTech-Pfizer nchini Uingereza na Marekani.

Soma zaidi: Marekani yaidhinisha chanjo ya pili ya COVID-19

Rais mteule wa Marekani Joe Biden alidungwa sindano ya kwanza kati ya mbili za chanjo hiyo, na kuonyeshwa kwenye televisheni. Amesema amefanya hivyo kuwahakikishia Wamarekani kuwa chanjo hiyo ni salama. Aliongeza kuwa kusambaza chanjo hiyo itachukua muda. Wakati huo huo, aliwataka raia wa Marekani kuvaa barakao na kuepuka safari zisizo za lazima katika kipindi cha Krismasi.

Vyanzo: (rtre,dpa,ap)