1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahl Köhler

Bettina Marx25 Mei 2009

Matokeo ya uchaguzi ni siku mbaya kwa chama cha SPD

https://p.dw.com/p/HwxI
Rais wa Ujerumani Horst KöhlerPicha: picture alliance/dpa

Rais wa Ujerumani, Horst Köhler, siku ya Jumamosi iliyopita amechaguliwa tena kushikilia wadhifa huo. Katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa hadhara kuu ya shirikisho, Bundesversammlung, rais Köhler alifaulu kupata wingi wa kura zilizohitajika kumpa ushindi dhidi ya wagombea wengine wa urais wa Ujerumani. Hii ina maana sasa Horst Köhler ataiwakilisha Ujerumani kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Yalikuwa matokeo yaliyokaribiana sana, lakini yalikuwa wazi vya kutosha. Wajumbe walidhihirisha wanachokitaka idadi kubwa ya Wajerumani. Kwa kuwa rais Köhler ambaye hakujulikana sana wakati alipochaguliwa mara ya kwanza, miaka mitano iliyopita, kuwa rais wa Ujerumani, sasa anafurahia uungwaji mkono mkubwa miongoni mwa Wajerumani wengi wanaompenda sana kiongozi huyo. Kama raia wa Ujerumani wangekuwa na uwezo kikatiba kumchagua rais wao, bila shaka wangempigia kura nyingi Hosrt Köhler, kwa mujibu wa kura za maoni ya wananchi zilizokusanywa. Asilimia 70 ya Wajerumani walioulizwa walipendelea rais Köhler aendelee kushikilia wadhifa wake kwa awamu ya pili.

Mpinzani wa karibu wa rais Köhler, Bibi Gesine Schwan, aliungwa mkono na asilimia 15 pekee ya Wajerumani katika kura za maoni, wakitaka achukue mahala pa rais Köhler kwa miaka mitano ijayo. Na hata katika hadhara kuu ya shirikisho, Bundesversammlung, Bi Gesine hakufaulu kupata kura za kutosha kuweza kumshinda rais Köhler. Hata katika kambi yake ya muungano wa chama cha Social Democratic, SPD, na chama cha Kijani, kulikosekana hatimaye kura 11 kwa profesa huyo wa maswala ya siasa.

Chama cha Christian Democratic Union, CDU na chama cha Federal Democratic, FDP, vimedhihirisha umoja kati yao vinaouhitaji ikiwa baada ya uchaguzi mkuu hapa Ujerumani mwezi Septemba mwaka huu, vitataka kuunda serikali mpya ya mseto. Chama cha SPD na cha Kijani ambavyo vinapania kuunda muungano, kwa upande wao vimedhihirisha, kwa mara nyengine tena, havina umoja, vimegawanyika na havitabiriki. Tayari kabla uchaguzi chama cha SPD kilikosekana katika kumuunga mkono Bi Gesine Schwan. Wanasiasa wa chama hicho walionekana kujitenga na kutokuwa na haja.

Lakini baada ya uchaguzi mwenyekiti wa chama cha SPD, Franz Münterfering, alitaka kukinyoshea kidole cha lawama chama cha Die Linke kwa kukikosoa kwamba kilijitenga. Badala ya kumuunga mkono mgombea wa chama cha SPD kwa wadhifa wa urais, Gesine Schwan, chama cha Die Linke kilikuwa na mgombea wake, na hivyo kudhoofisha kambi yao na kukipa nguvu chama cha CDU.

Ni kweli kwamba cha Kijani hakina makosa kwa kushindwa kwa mgombea wa chama cha SPD. Wanasiasa wa chama cha SPD wenyewe wanabeba dhamana kwa kushindwa kwa mgombea wao. Hakuna hata mara moja ambapo chama cha SPD kimeomba msaada kutoka chama cha Die Linke, kama alivyotangaza wazi kiongozi wa kundi la wabunge wa chama hicho, Gregor Gysi, wakati wa zoezi la kupiga kura kumchagua rais wa Ujerumani.

Hii ni kwa sababu chama cha SPD hakikutaka kuashiria kutaka kuunda serikali ya mseto na chama cha Die Linke na cha Kijani baada ya uchaguzi mkuu wa mwezi Septemba, na hivyo kuipa silaha kambi ya wahafidhina kuendesha kampeni kwamba kutakuja serikali ya kikomunisti. Kutarajia kwamba chama cha Die Linke kingekiunga mkono chama cha SPD ambacho kinafanya kila juhudi kujitenga nacho hadharani, ni kutozingatia hali halisi ya mambo au ni ufidhuli.

Sasa uchaguzi umekwisha na Ujerumani imepoteza nafasi yake ya kuwa na rais mzuri, mwanamke wa kwanza kushikilia wadhifa huo. Lakini wakati huo huo, Ujeruamni imejipatia tena rais mzuri anayependwa na watu, mnyenyekevu ambaye anaiwakilisha Ujerumani ndani na nje bila majivuno. Ilikuwa siku mbaya kwa chama cha SPD, lakini nzuri kwa Ujerumani.