1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

siku ya chakula duniani

Saumu Ramadhani Yusuf15 Oktoba 2010

Ulimwengu watakiwa kuongeza kilimo kupambana na tatizo la njaa

https://p.dw.com/p/PfHi
Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon Mkurugenzi mkuu wa shirika la (FAO) Jacques Diouf,Picha: picture-alliance / dpa

Rais wa Rwanda Paul Kagame ameutolea mwito ulimwengu kushikamana kupambana na njaa duniani.Akizungumza katika mkutano wa kimataifa kuhusu usalama wa chakula huko Roma italia rais huyo wa Rwanda ameitaka dunia kuelekeza juhudi  katika mikakati ya kuleta usalama wa chakula wakati ambapo takriban watu billioni moja wanakabiliwa na janga la njaa duniani.

Wakati ulimwengu ukijiandaa hapo kesho kuadhimisha siku ya chakula duniani, rais huyo wa Rwanda Paul Kagame ametoa mwito wa kuwepo mshikamo zaidi  katika kukabiliana na tatizo la ukosefu wa chakula na hasa katika ulimwengu wa nchi zinazoendelea barani Afrika.Aliuliza swali katika kikao hicho cha Roma akisema ikiwa kila mmoja anafahamu kwamba njaa inaua na kuwaondolea watu hadhi zao sasa kwanini hapachukuliwi hatua zaidi kukabiliana nayo?

Wito wake amezitaka nchi zote duniani kuelekeza  nguvu zao katika kupanga hatua zaidi za kuleta usalama wa chakula lakini pia ameonya  kwamba wakulima wadogo wasitengwe bali wahusishwe zaidi  katika kutafuta suluhisho. Zaidi ya hayo amezitahadharisha nchi za kiafrika ambako ndiko kwenye idadi kubwa ya watu wanaokabiliwa na njaa kwamba wasipotoshwe na kasumba kuwa sekta za binafsi  ndizo zinazoweza  kuchukua jukumu la kutatua tatizo hilo la njaa duniani-

Wakulima wadogo pamoja na familia zao  wanawakilisha  takriban idadi ya watu billioni 2 na nusu hii ikiwa ni zaidi ya thuluthi tatu ya idadi jumla ya watu duniani.Mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa mataifa linalohusika na masuala ya chakula na kilimo FAO Jacques Diof amesema janga la njaa duniani ni kitisho  cha usalama kwa jumla na kuzitaka serikali kuungana na kushirikiana  katika juhudi za kukabiliana na tatizo hilo.

Diof ameweka wazi katika kikao hicho kilichoandaliwa na shirika la FAO  mjini Roma kwamba kwa kila hali pana haja  ya kufikiwa malengo ya millenium ya kupunguza idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa kutoka idadi ya asilimia 20 ya  mwaka 1990  hadi asilimia 10 kufikia mwaka 2015.

Shirika la FAO  linakadiria kwamba  watu millioni 925 wanakumbwa na baa la njaa ikilinganishwa na watu billioni zaidi ya moja mwaka jana kutokana na athari zilizosababishwa na  kuporomoka kwa uchumi pamoja na kupanda kwa bei ya vyakula katika mwaka wa 2007 hadi mwaka 2008.

Aidha serikali zimetakiwa kuwasaidia wanawake ambao zaidi ndio wanaolima vyakula kwa wingi katika nchi zinazoendelea  lakini haviwafaidishi.Wanawake pia wametakiwa kuwa mfano katika mapambano dhidi ya njaa duniani.

Mwandishi Saumu Mwasimba/AFPE 

Mhariri AbdulRahaman