1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya kimataifa ya uhuru wa vyombo vya habari

3 Mei 2016

Ulimwengu unaadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani. Maadhimisho hayo yanafanyika mjini Helsinki, Finland yakiongozwa na shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO.

https://p.dw.com/p/1Iguu
Nembo ya Siku ya kimataifa ya Uhuru wa vyombo vya habari

Ni siku ambayo dunia inatathmini hali ya uhuru wa vyombo vya habari duniani kote, ambapo inatolewa michango ya kutetea vyombo vya habari vinavyokabiliana na mashambulizi pamoja na kuwakumbuka waandishi habari waliopoteza maisha yao wakiwa kazini.

Kila mwaka zaidi ya maadhimisho 100 ya kitaifa yanafanyika kuiadhimisha siku hii. Na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO ndilo linaloongoza maadhimisho hayo katika kila pembe ya dunia. Kauli mbiu ya siku hii kwa mwaka huu ni "upatikanaji wa habari na uhuru wa kimsingi."

Uhuru wa Habari na Malengo ya Maendeleo Endelevu

Katika taarifa ya UNESCO iliyochapishwa kwenye tovuti yao, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Irina Bokova amesema:"Mwaka 2015 dunia ilipitisha malengo 17 ya maendeleo endelevu. Ili kuhakikisha kunafanyika juhudi zaidi katika miaka 15 ijayo za kukomesha umaskini, kuhakikisha ustawi kwa wote, kuilinda dunia, pamoja na kuendeleza amani. Tunaweza kufikia malengo hayo iwapo tutafanya kazi kwa pamoja na kama tutakuwa na taarifa zenye ubora. Kutokana na hayo ndio maana siku ya uhuru wa vyombo vya habari ya 2016 inayozinduliwa mjini Helsinki, imeamua kuonyesha umuhimu wa uandishi wa habari ulio huru katika kutekeleza ajenda ya maendeleo endelevu yanayotegemewa kutekelezwa ifikapo mwaka 2030."

Südafrika Johannesburg Protest Pressfreiheit
Maandamano kudai Uhuru wa Yyombo vya Habari Johannesburg-Afrika KusiniPicha: Julie Reid

Shirika la UNESCO pamoja na serikali ya Finland wanashirikiana kuandaa sherehe kuu ya siku ya leo pamoja na sherehe ya tuzo ya UNESCO ya Guillermo Cano kwa mwaka 2016, zitakazofanyika kwa pamoja katika mji mkuu Helsinki na zinategemewa kumalizika tarehe 6.

Tuzo ya Guillermo Cano kwa Mwandishi habari wa Azerbaijan

Khadija Ismayilova, mwandishi wa habari za uchunguzi kutoka Azerbaijan, ndiye aliyechaguliwa kupokea tuzo ya mwaka huu ya Guillermo Cano ya UNESCO.

Türkei Istanbul Demonstration für Pressefreiheit
Maandamanon ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Istanbul-UturukiPicha: Getty Images/AFP/O. Kose

Ismayilova, ni mwandishi wa kujitegemea na mchangiaji wa idhaa ya Azerbaijani ya Radio Huru ya Ulaya. Desemba mwka 2014 aliwekwa kizuizini na Septemba 2015, alihukumiwa kifungo cha miaka saba na nusu kwa tuhuma zinazohusiana na matumizi mabaya ya madaraka na ukwepaji wa kodi.

Tuzo hiyo ilianzishwa kwa mara ya kwanza na Halmashauri Kuu ya shirika la UNESCO mwaka 1997. Na hafla hiyo ya kila mwaka inatoa tuzo ya heshima kwa mtu, shirika au taasisi yoyote ambayo imechangia pakubwa katika masuala ya utetezi na, kukuza uhuru wa vyombo vya habari mahali popote duniani

Halikadhalika siku hii ya kimataifa ilitangazwa katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 1993 kufuatia pendekezo liloyopitishwa katika Kikao cha 26 cha Mkutano Mkuu wa UNESCO wa mwaka 1991.

Siku ya uhuru wa vyombo vya habari mwaka huu inaonyesha uhusiano kati ya uhuru wa vyombo vya habari, utamaduni wa kuwepo kwa uwazi na haki ya uhuru wa habari, na maendeleo endelevu katika karne ya mawasiliano ya digitali. Suala moja muhimu katika haya yote ni jukumu la uandishi wa habari, na umuhimu wa kuwalinda wale ambao wanahusika na taaluma hii inayohudumia umma kwa kuwaletea habari zinazoendelea duniani kote.

Mwandishi: Yusra Buwayhid

Mhariri:Yusuf Saumu