1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya mwisho ya kuwasilisha fomu kuwania urais Afghanistan

7 Mei 2009

Huko nchini Afghanistan leo ndiyo siku ya mwisho kwa wagombea urais kuchukua fomu na kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa tarehe 20 August.

https://p.dw.com/p/HlYr
Ramani inayoonesha Afghanistan na PakistanPicha: DW

Tayari kuna ishara wazi kuwa upande wa upinzani dhidi ya Rais wa sasa Hamid Karzai unajaribu kuungana kumuunga mkono mgombea mmoja.Hata hivyo bado rais huyo anaoneka kuwa katika nafasi nzuri ya kushinda, kutokana na kuwepo kwa wagombe wengi upande wa upinzani.


Waziri wa zamani wa fedha wa nchi hiyo Ashraf Ghani pamoja na waziri wa zamani wa mambo ya nje Abdullah Abdullah walijisajili hapo jana na kuongeza uzito katika upinzani dhidi ya Rais Karzai,na kufikisha idadi wagombea 24 waliyojitokeza kuwania nafasi hiyo kabla ya muda kumalizika hii leo.


Hamid Karsai warnt Pakistan vor Angriffen
Rais Hamid KarzaiPicha: AP

Hatua hiyo inaonekana kupunguza kura za upinzani dhidi ya Rais Karzai ambaye amekuwa madarakani toka mwaka 2001.Rais Karzai yeye aliwasilisha fomu zake za kugombea hapo siku ya Jumatatu kabla ya kuelekea Marekani alikuwa na mazungumzo na Rais Barack Obama pamoja na Rais wa Pakistan Asif Ali Zardari.


Mmoja wa wapinzani wakubwa wa Rais Karzai Gul Agha Sherzai alitangaza kujitoa katika mbio hizo, kumuunga mkono kiongozi huyo, ambapo kwa upande mwengine upinzani mpaka sasa umeshindwa kukubaliana kuungana na kuwa na mgombea mmoja.


Akizungumza mara baada ya kuwasilisha fomu zake Waziri huyo wa zamani wa fedha,na mkuu wa zamani wa chuo kikuu, Ashraf Ghani alisema kuwa anawania nafasi hiyo ingawa anaamini kuwa hakutakuwa na usawa na haki katika uchaguzi huo.


Amesema kuwa kwa sasa nguvu zote za serikali, ikiwa ni pamoja na ushawishi vinatumika kumuunga mkono Rais Karzai.


Ghani ambaye kama alivyo Rais Karzai anatoka katika kabila la wapashtuni ambalo ni kubwa nchini Afghanistan, na alikuwa Waziri wa Fedha chini ya utawala wa Rais Karzai katika kipindi cha mwaka 2002 na 2004.


Msomi na mwanazuoni huyo anayeheshimika kimataifa, ni mkongwe wa utawala wa zamani uliyoondoshwa madarakani wa Taliban.


Anaaminika kuwa mmoja wa wagombea ambao wamekuwa katika mazungumzo na wagombea wengine kuangalia jinsi ya kuungana na kuwa na mgombea mmoja ambaye ataweza kuungwa mkono na makundi yote ya kikabila nchini humo.


Naye Abdullha Abdullah waziri wa zamani wa Mambo ya Nje ambaye ni nusu mpashtun na nusu kabila dogo la watajik, alikuwa na uhusiano wa karibu kwa muda mrefu na kiongozi wa wanamgambo wa mujahidden wa kabila hilo la Tajik kamanda Ahmad Shah Masood.


Kamanda Massod aliuawa kwa bomu katika ngome yake na watu waliyojifanya waandishi wa habari enzi za utawala wa Taliban nchini Afghanistan.


Mapema, kamanda wa zamani wa Taliban Abdul Salam Rocketi pia aliwasilisha fomun zake kuwania kiti hicho


Kamanda huyo alibatizwa jina hilo la Rocketi kutokana na uwezo wake mkubwa wakati wa vita dhidi ya uvamizi wa Urusi kwenye miaka ya 80.


Alikuwa mmoja wa wanachama wa juu wa Taliban kuanzia mwaka 1986 hadi mwaka 2001 na alitumikia kifungo cha miaka miwili jela baada ya utawala huo wa Taliban kuangushwa.


Mwengine ambaye ameamua kuingia katika mbio hizo ni waziri wa zamani wa Ulinzi enzi za ukoministi Shahnawaz Tanai ambaye aliongoza mapinduzi yaliyoshindwa mwaka 1990 na ambaye inasemekana ana maingiliano makubwa na Pakistan.


Wagombea wote wa urais huo wa Afghanistan watafanyiwa usaili kuhakikisha wanakidhi taratibu na sheria za kuwa mgombea, kama kuwa raia wa Afghanistan, kuwa muislam pamoja na umri siyo chini ya miaka 40.


Uchaguzi huo wa tarehe 20 August unaonekana kuwa mtihani muhimu kwa jitihada za nchi za magharibi kuhakikisha kunakuwepo demokrasia nchini humo, na kuliondoa taifa hilo kutokana katika ushawishi wa watu wenye kufuata misingi ya imani kali za kidini na nchi isiyo na sheria.


Kiasi cha watu 1,575 wakiwemo wanawake 178 mpaka sasa wamejiandikisha kuwania viti 420 vya bunge la nchi hiyo.Robo ya viti hivyo vimetengwa kwa ajili ya wanawake.

Mwandishi:Aboubakary Liongo

Mhariri:Mohamed Abdul-Rahman