1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya Ukimwi duniani

1 Desemba 2015

Tarehe mosi Desemba ni siku ya Ukimwi duniani, siku ambayo imetegwa na Umoja wa Mataifa kutafakari na kuwakumbuka wale wote waliopoteza maisha yao kutokana na ugonjwa huu.

https://p.dw.com/p/1HFBi
Alama ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi duniani
Picha: ANTONIO SCORZA/AFP/Getty Images

Viongozi wa dunia kwa kauli moja wameeleza nia yao ya kutaka kuutokomeza kabisa ugonjwa wa Ukimwi ifikapo mwaka 2030 kama sehemu ya malengo endelevu ya maendeleo yaliyopitishwa mwezi Septemba mwaka 2015.

Nia hii inaakisi nguvu ya mshikamano, kupambana na ugonjwa huo, lakini mpango wa umoja wa mataifa wa kupambana na ugonjwa huo umeonya juu ya kuonesha hali ya kufurahia ushindi.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema kwamba watu milioni 15 tayari wanapata matibabu ya kuokoa maisha yao kutokana na maambukizi ya HIV.

Maambukizi yapungua

Maambukizi mapya yamepungua kwa asilimia 35 tangu mwaka 2000 na vifo vinavyohusiana na ugonjwa wa Ukimwi vimepungua kwa asilimia 42 duniani kote tangu ugonjwa huo kushika kasi mwaka 2004.

Dunia imo katika kasi ya kuutokomeza ugonjwa huo wa Ukimwi. Ili kuutokomeza kabisa ugonjwa wa Ukimwi ifikapo mwaka 2030 kama sehemu ya malengo endelevu ya maendeleo kutahitajika kuharakishwa uwekezaji, nia thabiti na ubunifu.

Siku ya Ukimwi duniani nchini China
Siku ya Ukimwi duniani nchini ChinaPicha: picture-alliance/dpa

Mtazamo wa kasi ya utokomezaji wa Ukimwi kama ulivyoanishwa na shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na ugonjwa huo UNAIDS, ni pamoja na uwekezaji, malengo kuelekea maeneo, jamii na mipango ambayo italeta mafanikio makubwa.

Kuna pia kuushirikisha uongozi wa maeneo husika kwa ajili ya hatua endelevu za kuchukuliwa na uwajibikaji. Hata hivyo katika mkesha wa siku ya Ukimwi duniani, mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na Ukimwi UNAIDS, Simon Bland, amedokeza kwamba ni mapema mno kushangiria ushindi dhidi ya ugonjwa huo.

"Siku ya Ukimwi duniani, ni wakati muhimu wa kutafakari na kuwakumbuka wale wote waliopoteza maisha yao kutokana na ugonjwa huu. Ni fursa ya kujiangalia, fursa ya kutafakari kuhusiana na changamoto ambazo tunakumbana nazo leo hii, na siku sijazo, na pia ni fursa kwa dunia kuja pamoja katika kuutokomeza ugonjwa huu ifikapo mwaka 2030 kama ilivyoainishwa katika malengo endelevu ya maendeleo."

Kiongozi wa Kanisa katoliki Papa Francis akiwa mjini Bangui, Afrika ya Kati.
Kiongozi wa Kanisa katoliki Papa Francis akiwa mjini Bangui, Afrika ya Kati.Picha: Getty Images/AFP/G. Guercia

Hatua za haraka lazima zichukuliwe

Bland amewaambi bia waandishi habari kwamba maambukizi ya HIV sio tena hukumu ya kifo, iwapo unaishi katika nchi ambazo uwezekano wa kupata matibabu na huduma upo. Lakini ameongeza hatuwezi kuchukulia suala hili kuwa ni la bahati tu.

Tunapaswa kuharakisha na kuongeza kasi ya hatua tunazochukua, iwapo tunataka kuwapatia wale wote wenye mahitaji ya huduma na matibabu huduma hizo.

Kiongozi wa kanisa Katoliki Papa Francis nae amekiri jana kwamba suala la iwapo kanisa liruhusu matumizi ya mipira ya kondomu katika mapambano dhidi ya maambukizi ya HIV na Ukimwi, lina utata, lakini amesema dunia ina matatizo mengine makubwa zaidi.

Mwandishi: Sekione Kitojo/afpe

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman