1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya Wafanyakazi Duniani

30 Aprili 2010

Tarehe mosi Mei ni siku ya wafanyakazi inayoadhimishwa katika nchi mbali mbali duniani. Desturi hiyo ilianza miaka 120.

https://p.dw.com/p/NAlo

Tarehe 14 Julai mwaka 1889, mkutano wa kimataifa wa wafanyakazi mjini Paris uliamua kuwa na siku maalum ambapo wafanyakazi wataweza kufanya maandamano kudai kufanya kazi saa nane kwa siku. Kwa vile jumuiya ya wafanyakazi nchini Marekani tayari iliamua kuwa na maandamano kama hayo tarehe mosi Mei mwaka 1890, basi siku hiyo ikachaguliwa.

Tangu wakati huo tarehe mosi Mei ni maarufu kama siku ya vyama vya wafanyakazi, lakini ikaja kupoteza heba yake. Kwani nchini Ujerumani mafashiti waliitangaza tarehe hiyo siku kuu rasmi na wakaitumia kwa propaganda zao na kufanya maandamano makubwa ya umma huku waakilishi wa vyama vya wafanyakazi wakitoweka jela au kambi za mateso. Hata nchi za kambi ya Mashariki ziliitumia vibaya siku hiyo ya wafanyakazi. Ilitumiwa kuonyesha nguvu za kijeshi, kuanzia gwaride la majeshi,vifaru na makombora, wakati vyama vya wafanyakazi vikifanywa vyombo vya serikali na vyama vya kisiasa.

Je, Mei mosi mwaka 2010 ikoje? Mwaka huu, shirikisho la vyama vya wafanyakazi vya Ujerumani, DGB, limeachana na kauli mbiu "Tunasonga Mbele." Kwa mujibu wa DGB, safari hii mada ya kukabiliana na mizozo ya ajira inapewa kipaumbele katika maandamano yao. Kwa sehemu kubwa, vyama vya wafanyakazi na mabaraza ya waakilishi wa waajiriwa yalichangia kudhibiti ukosefu wa ajira. Wajumbe hao walipigania mpango wa kufupisha saa za kufanya kazi, mikataba ya mishahara inayosaidia kuhifadhi ajira na mipango ya kuimarisha uchumi. Sasa ni wakati wa kuhakikisha usalama wa ajira na kuimarisha makampuni.

Wale waliosababisha msukosuko wa kiuchumi wanapaswa kuwajibika na kuchukua hatua za kuimarisha sekta za ajira, elimu na jamii. Hiyo ni kauli mbiu ya tarehe mosi Mei. Lakini wanaopaza sauti wanazidi kupunguka kwani wanachama wanajitoa kama ilivyo kanisani na katika klabu za spoti. Chama cha zamani cha wafanyakazi wa iliyokuwa Ujerumani ya Mashariki, FDGB, kilipovunjwa mwaka 1990 na kujiunga na DGB, walikuwepo wanachama milioni kumi na moja. Mwaka 2001 idadi yao ilipunguka hadi milioni 7.8 na mwaka uliopita iliangukia milioni 6.3 tu.

Mwandishi: Wenkel,Rolf/ZPR/P.Martin

Mhariri: Othman, Miraji