1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya wakimbizi ulimwenguni

Mwadzaya, Thelma20 Juni 2008

Leo ni siku ya wakimbizi Ulimwenguni.Lengo la maadhimisho ya siku hii ni kuangazia hali ya wakimbizi na watu walioachwa bila makazi kote ulimwenguni.

https://p.dw.com/p/ENQc
Antonio Guterres, Kamishna wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCRPicha: picture-alliance/ dpa


Yapata watu milioni 40 kote ulimwenguni wanazongwa na tatizo hili linalosababishwa na vita vinavyoambatana na mateso.Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni usalama kwa wakimbizi.Kwa mujibu wa Kamishna wa Tume ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa wakimbizi milioni 11.4 walisajiliwa mwaka jana.Idadi hiyo imeongezeka kutoka milioni 9.9 mwaka 2006.


Nchi za Uchina,India,Malaysia,Thailand na Bangladesh zimeripotiwa kuwa nchi zilizo na ukiukaji mkubwa wa haki za wakimbizi kote ulimwenguni..Mataifa mengine yaliyoorodheshwa ni Iraq,Kenya,Urusi ,Sudan na Bara la Ulaya.Utafiti huo wa kila mwaka ulifanywa na Kamati ya Marekani inayohusika na masuala ya Wakimbizi na Wahamiaji, USCRI.Takwimu za Shirika hilo lisilo la kiserikali zinaonyesha kuwa mwishoni mwa mwaka jana idadi ya wakimbizi iliongezeka hadi milioni 14 na kuelezwa kuwa ongezeko kubwa zaidi tangu mwaka 2001.


Kurejeshwa kwa lazima


Wakimbizi kutoka nchi ya Iraq wanaripotiwa kuongezeka na kufikia laki tano u nusu waliokimbia nchi yao.Zaidi ya wakimbizi milioni mbili wanasubiri ghasia kumalizika nchini mwao ndipo waweze kurudi zinaeleza takwimu hizo.


Orodha hiyo ilizingatia vigezo vya namna nchi husika zinavyowashughulikiwa wakimbizi.Baadhi ya nchi ziliwalazimisha wakimbizi kurejea walikotoka ambako wanakabiliwa na tishio la kuteswa au kuuawa kwa upande mmoja ..kwa upande mwingine wakimbizi hao waliwaruhusu wakimbizi hao kuingia nchini mwao ila kuwaacha kubakia katika kambi zinazokabiliwa na uhaba wa vifaa na bidhaa za matumizi.Hayo ni kwa mujibu wa Kiongozi wa Shirika hilo la USCRI Lavinia Limon.


Ghasia na vita


Vita vinachangia katika ongezeko la wakimbizi barani Afrika,Asia na Mashariki ya kati vilevile kutatiza juhudi zinazofanywa na mashirika ya misaada za kupambana na tatizo hilo.Akizungumza hapo jana katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab kaskazini mwa Kenya Kamishna wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR Antonio Guterres alisema


''Tunajitahidi lakini tunahitaji fedha zaidi za kufadhili miradi ya kuwahudumia wakimbizi.''


Kambi ya Dadaab inawahifadhi wakimbizi kutoka nchi jirani ya Somalia inayozongwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu kungolewa madarakani kwa Rais Siad Barre mwaka 1991.Yapata watu milioni moja wameachwa bila makazi tangu vita kati ya wapiganaji wa Kisomali na wanajeshi wa serikali ya mpito ya Somalia wakishirikiana na Ethiopia kuanza mwanzoni mwa mwaka jana.Maelfu wamepoteza maisha yao katika ghasia hizo. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa wakimbizi alfu 4 wa Kisomali wanaingia nchini Kenya kila mwezi na kupokelewa katika kambi ya Dadaab


Kwa sasa idadi hiyo imefikia laki mbili.Kambi hiyo pia inahifadhi wakimbizi kutoka mataifa ya Uganda,Congo,Ethiopia na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.Bwana Guterres aliongeza kuwa wakimbizi laki moja na kumi wa Somalia wanapata hifadhi nchini Yemen ila idadi hiyo inaongezeka.


Katika maadhimisho ya siku ya Wakimbizi Ulimwenguni Kamishna wa Tume ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anazuru eneo la Kusini mwa Sudan ili kushuhudia hali halisi inayowakumba wakimbizi barani Afrika.


Mataifa ya magharibi ikiwemo Marekani na wanchama wa Umoja wa Ulaya yamelaumiwa katika ripoti hiyo kwa kuwarudisha nyumbani kwao kwa lazima baadhi ya wakimbizi.