1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Silaha nzito kuanza kuondolewa mashariki ya Ukraine

22 Februari 2015

Waasi wanaoiunga mkono Urusi wamesema wataanza kundowa silaha zao nzito kutoka medani ya mapambano Jumapili(22.02.2015) lakini serikali imesema msafara wa magari ya kijeshi umevuka mpaka kutoka Urusi kuingia Ukraine.

https://p.dw.com/p/1Efm3
Wanajeshi wa serikali mashariki mwa Ukraine.
Wanajeshi wa serikali mashariki mwa Ukraine.Picha: Reuters/G. Garanich

Jeshi la Ukraine limesema waasi wamekuwa wakiendelea na mashambulizi dhidi ya vikosi vya serikali karibu na Mariupol mji wa bandari ulioko kwenye mikono ya serikali ambao unaonekana kuwa ndio utakaokuwa shabaha kuu mpya ya mashambilizi hayo ya waasi.

Msemaji wa jeshi la Ukraine Andry Lysenko amesema treni ya kijeshi iliokuwa imebeba magari sitini ya kivita vikiwemo pia vifaru imewasili katika mji wa Amvrosivka kutoka Urusi hapo Jumamosi. Baadae msafara wa zana za kijeshi ulivuka mpaka karibu na Novoazovck mashariki mwa Mariupol katika Bahari ya Azov.

Amesema mapigano yamekuwa yakiendelea katika kijiji cha Shyrokyne mashariki mwa Mariupol ambapo amesema kumekuwepo na jumla ya mashambulizi 44 yaliofanywa na waasi katika eneo la mzozo kwenye kipindi cha masaa 24 yaliyopita.

Katika mji wa Kharkiv watu watatu wameuwawa Jumapili na kumi kujeruhiwa wakati kifaa cha mripuko kilipovurumishwa kwa watu waliokuwa kwenye maandamano ya amani.

Kuheshimiwa kwa suluhu

Kamanda wa waasi wanaoiunga mkono Urusi amesema waasi hao wanatazamiwa kuanza kuondowa silaha zao nzito kutoka eneo la mapambano mashariki mwa Ukraine Jumapili jambo ambalo ni ishara kuwa waasi wako tayari kusitisha mashambulizi yao ya kusonga mbele kama sehemu ya kuzingatia makubaliano ya amani ya kimataifa.

Waasi wanaoiunga mkono Urusi mashariki mwa Ukraine.
Waasi wanaoiunga mkono Urusi mashariki mwa Ukraine.Picha: Reuters/B. Ratner

Mapigano yalipunguwa katika maeneo mengi tokea usitishaji wa mapigano uanze kufanya kazi wiki moja iliopita lakini suluhu hiyo imeyumba kutokana na hatua ya waasi kuuteka mji wa Debaltseve hapo Jumatano na kuwalazimisha maelfu ya wanajeshi wa Ukraine kurudi nyuma.

Hatua za kuondowa silaha nzito pamoja na ile ya kubadilishana wafungwa hapo Jumamosi na serikali ya Ukraine yumkini ikawa inaashira kwamba waasi hao wanakusudia kuheshimu suluhu hiyo kikamilifu baada ya kufanikisha lengo lake la kijeshi la kuuteka mji wa Debaltseve.

Kuondolewa silaha nzito

Shirika la habari la Urusi Interfax limemnukuu kamanda wa waasi Eduard Basurin akisema kwamba mpango huo umesainiwa Jumamosi usiku ili uanze Jumapili ambapo wana wiki tatu za kuondowa silaha hizo nzito.

Kamanda wa waasi Eduard Basurin.
Kamanda wa waasi Eduard Basurin.Picha: Reuters/M. Shemetov

Shirika jengine la habari la Urusi TASS limemkariri akisema uondowaji wa silaha hizo bado uko kwenye maandalizi na kwamba uondowaji hasa wa silaha hizo utaanza Jumanne.

Shuhuda mmoja wa shirika la habari la Uingereza Reuters ameona msafara wa magari 20 ya kijeshi ya waasi yakiwa yamepakia mizinga ya kudungulia ndege na makombora ukiondoka Debaltseve na kuelekea Donetsk.

Wasi wasi wa kushambuliwa Mariupol

Shambulio lolote lile dhidi ya mji wa Mariupol wenye wakaazi nusu milioni na njia kuu ya kuingilia Crimea ambayo Urusi imeinyakuwa mwezi wa Machi mwaka jana itauwa kabisa makubaliano hayo ya kusitisha mapigano.

Mwanamgambo wa serikali akiwa katika mji wa Mariupol.
Mwanamgambo wa serikali akiwa katika mji wa Mariupol.Picha: Philippe Desmazes/AFP/Getty Images

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ameionya Urusi dhidi ya kuchochea zaidi mgogoro wa Ukraine, akisema mashambulizi ya waasi kwenye mji wa Mariupol yatakuwa ukiukwaji wa wazi wa makubaliano ya amani yalioungwa mkono na jamii ya kimataifa.

Katika mahojiano na gazeti linalosomwa na watu wengi zaidi nchini Ujerumani la Bild, kwa ajili ya toleo la Jumatatu, Steinmeier ambaye yuko nchini Kenya akikamilisha ziara yake ya mataifa matatu ya Afrika, amesema hatua yoyote ya kusonga mbele kwenye mji wa Mirupol itakuwa ukiukaji wa makubaliano ya Minsk.

Uwezekano wa vikwazo vipya kwa Urusi

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema siku ya Ijumaa kuwa vikwazo vipya dhidi ya Urusi vitazingatiwa ikiwa makubaliano hayo ya amani yatakiukwa.

Hapo Jumamosi waasi na serikali walibadilishana takriban wafungwa 200 ikiwa ni mojawapo ya hatua za mwanzo kutekeleza makubaliano hayo ya amani yaliofikiwa mwezi wa Februari katika mji mkuu wa Belarus Minsk baada ya viongozi wa Ujerumani,Ufaransa, Urusi na Ukraine kukutana katika juhudi za kukomesha mzozo huo wa miezi kumi.

Serikali ya Ukraine inawashutumu waasi kwa kuandaa vikosi vyake na silaha kusini mashariki kwa Ukraine kwa uwezekano wa kuushambulia mji wa Mariupol ambapo vikosi vya serikali vinajiandaa kulizima.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters

Mhariri : Iddi Ssessanga