1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Silaha za kemikali zilitumika Syria

Carolyne Robi26 Aprili 2013

Marekani imesema serikali ya Assad ilitumia silaha za kemikali katika vita nchini Syria lakini imesisitiza kuwa Rais Barrack Obama anahitaji ushahidi zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote.

https://p.dw.com/p/18NdF
SyriaPicha: Reuters

Taarifa hizo kutoka ikulu ya Rais ya white house kuwa kulitumika silaha za kemikali Syria kulizua miito kutoka kwa baadhi ya wabunge Marekani kuwa utawala wa Obama unastahili sasa kuchukua hatua za kijeshi jambo ambalo Rais Obama amekuwa akiepuka kufanya.

Serikali ya Marekani inaonekana kubadili msimamo wao kuhusiana na madai hayo ya matumizi ya silaha za sumu na sasa maafisa wa ikulu wamesema asasi za kijasusi zinaamini kuwa sumu aina ya sarin ilitumiwa na majeshi ya Assad dhidi ya waasi lakini bado masuala fulani yanahitaji ufafanuzi.

Waziri wa ulinzi wa Marekani Chuck Hagel
Waziri wa ulinzi wa Marekani Chuck HagelPicha: Saul Loeb/AFP/Getty Images

Waziri wa ulinzi wa Marekani Chuck Hagel amesema huenda majeshi ya Syria yalitumia silaha za sumu katika vita vinavyoendelea nchini humo na marekani haiwezi thibitisha zilikotoka silaha hizo lakini iinaamini majeshi ya Assad yalitumia.

Utawala wa Obama wachukua tahadhari

Licha ya Rais Obama kutangaza kuwa matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria itakuwa mwanzo wa kuchukuliwa kwa mkondo mpya wa vita hivyo, na kutishia kuchukua hatua kali iwapo zitatumika, utawala wake unaonekana kuwa makini katika kuchukua hatua zozote ikisema inazingatia mafunzo nchi hiyo ilipata kuhusu hali ilivyokuwa katika kuanza kwa vita vya Iraq karibu muongo mmoja uliopita.

Wakati huo utawala wa Rais George W. Bush ulitumia taarifa za kijasusi ambazo hazikuwa sahihi kuivamia Iraq kutafuta silaha za kinyuklia, kemikali na za kibayolojia ambazo baadaye ilikuja kubainika kuwa hazikuwepo.

Rais wa Marekani Barrack Obama
Rais wa Marekani Barrack ObamaPicha: picture-alliance/dpa

Mkurugenzi wa afisi ya masuala ya kisheria wa Ikulu ya Marekani, Miguel Rodriguez, amewaandikia barua wabunge nchini humo akisema kuwa kutokana na hali ilivyo na kujifunza kutoka makosa ya vita vilivyopita, tathimini za kijasusi pekee hazitoshi bali hali halisi ya kuaminika na kuthibitishwa ndiyo itaongoza kuafikia maamuzi.

Sarin ilitumika kati vita vya Iraq

Wataalamu wa silaha za kemikali wanasema sarin kemikali inayoathiri mfumo wa neva inaweza kutambulika katika mwili wa binaadamu kupitia damu, mkojo au kwa sampuli ya nywele ama hata kwa mchanga na matawi ya sehemu ilipotumika.

Inasemekana Iraq ilitumia sumu hiyo ya sarin miaka 25 iliyopita dhidi ya mji wa Wakurdi wa Halabja wakati wa vita kati ya Iraq na Iran. Mnamo mwaka 1994 ilitumika na kundi la kidini la itikadi kali dhidi ya wasafiri wa reli mjini Tokyo.

Marekani imekuwa ikiepuka kuingizwa moja kwa moja katika vita vya Syria kutoa usaidizi wa kijeshi na imekuwa ikitoa misaada isiyokuwa ya silaha kwa waasi wanaotaka kumng'oa madarakani Rais Assad.

Mtambo wa kemikali za sumu
Mtambo wa kemikali za sumuPicha: picture-alliance/dpa

Marekani ina wasiwasi kuwa kupewa silaha kwa waasi huenda zikaishia kwa mikono ya magaidi walio na mafungamano na mtandao wa Al Qaeda.

Maoni yanayoungwa mkono na Ujerumani ambayo imesema baadhi ya raia wake wenye misimamo mikali ya kidini wanashiriki katika vita hivyo vya Syria, siku moja baada ya Umoja wa Ulaya kuonya kuwa wapiganaji hasa kutoka Uingereza, Ufaransa na Ireland wanapigana Syria dhidi ya utawala wa Assad.

Mwandishi: Caro Robi/ Reuters/dpa

Mhariri: Josephat Charo