1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Silaha za kikemia zashukiwa kutumiwa Syria

20 Machi 2013

Kumekuwepo kushutumiana baina ya serikali ya Syria na waasi wanaoipinga, kila upande ukiutuhumu mwingine kutumia silaha za kikemia katika mashambulizi yaliyouwa watu zaidi ya 30 karibu na mji wa Aleppo jana.

https://p.dw.com/p/180WT
Serikali na waasi wanalaumiana kutumia silaha za kikemia
Serikali na waasi wanalaumiana kutumia silaha za kikemiaPicha: Reuters

Shirika la habari la Syria limetangaza kuwa magaidi wamefyatua silaha za kikemia katika eneo la Khan al-Assal katika mkoa wa Aleppo, na waziri wa habari Omran al-Zohbi amesema mashambulizi hayo yanazusha hali ya hatari. Naibu waziri wa mambo ya nchi za nje wa nchi hiyo Faisal Muqdad amesema kuwa watu 31 wameuawa katika mashambulizi hayo, ambayo pia yamewajeruhi wengine zaidi ya 100.

Kituo cha taifa cha televisheni kilionyesha magari ya kubeba wagonjwa yakiwasilisha majeruhi katika hospitali ya mjini Aleppo, na madaktari wamesema kuwa gesi ya sumu ilitumiwa katika mashambulizi dhidi ya watu hao.

Kila upande waushutumu mwingine

Waasi wamekanusha kuhusika na mashambulizi hayo, na badala yake wameishutumu serikali kutumia makombora ya masafa marefu, ambayo yanasababisha matatizo ya kupumua. Mwenyekiti wa kongamano la kitaifa la Syria Moaz al-Khatib amekanusha uwezekano kwamba upinzani unaweza kutumia silaha hizo.

''Bado hatujapata maelezo kamili, lakini tunapinga matumizi ya silaha za kikemia kutoka pande zote. Sitarajii kwamba wanamapinduzi wanaweza kutumia silaha hizo, na tunapinga upande wowote kuzitumia.'' Amesema al-Khatib.

Mwanamke aliyejeruhiwa katika mashambulizi ya kutumia ''silaha za kikemia''
Mwanamke aliyejeruhiwa katika mashambulizi ya kutumia ''silaha za kikemia''Picha: Reuters

Shirika la kutetea haki za binadamu nchini Syria ambalo lina makao yake nchini Uingereza limeripoti kuwa waasi walikishambulia kituo cha jeshi la serikali kwa makombora na kuuawa askari 16 na raia 10, lakini halikusema iwapo makombora hayo yalikuwa na silaha za kikemia.

Mataifa makubwa yafuatilia

Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Urusi imesema inazo taarifa kutoka mjini Damascus kwamba waasi wametumia silaha za kikemia, na kuelezea wasiwasi wake kwamba kuwepo kwa silaha hizo katika kile ilichokiita ''mikono isiyo salama'' kunaifanya hali ya mgogoro wa Syria kuwa ngumu zaidi.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Jay Carney amesema serikali mjini Washington haina ushahidi kuthibitisha kwamba waasi nchini Syria wametumia silaha za aina hiyo, na msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya nchi hiyo Victoria Nuland ameongeza kuwa balozi wao nchini Urusi atataka ufafanuzi kutoka serikali ya mjini Moscow.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameonya kuwa matumizi ya silaha Syria yatakuwa uhalifu mkubwa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameonya kuwa matumizi ya silaha Syria yatakuwa uhalifu mkubwa.Picha: Reuters

Ban atoa onyo

Tangazo kutoka Umoja wa mataifa kuhusiana na suala hilo, limeelezea maoni ya katibu mkuu wa Umoja huo, kwamba kutumiwa kwa silaha hizo na upane wowote katika mgogoro wa Syria kutachukuliwa kama uhalifu mkubwa.

Nayo serikali ya Uingereza imeonya kwamba iwapo madai hayo ya kutumiwa kwa silaha za kikemia yatathibitishwa, itaangalia upya msimamo wake kuhusu mgogoro wa Syria ambao umedumu kwa miaka miwili sasa.

Wakati huo huo kamanda mkuu wa umoja wa kujihami, NATO, James Stavridis amesema mjini Washington kwamba umoja huo unatafakari uwezekano wa kuingilia kijeshi nchini Syria. Hata hivyo kamanda huyo amesema kuwa hatua yoyote itachukuliwa ikiwa itaafikiwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, na kukubaliwa na wanachama wote 28 wa umoja huo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE

Mhariri: Josephat Charo