1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sintofahamu katika kikao cha AU

Thelma Mwadzaya4 Februari 2009

Umoja wa Afrika umerefusha kikao chake katika mkutano wake wa kilele mjini Addis Ababa baada ya kushindwa kuafikiana kuhusu suala la kuunda shirikisho la mataifa ya bara la Afrika.

https://p.dw.com/p/GmsO
Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika AU Kanali Muammar GaddafiPicha: AP


Pendekezo hilo liliwasilishwa na mwenyekiti mpya wa Umoja huo kiongozi wa Libya Muammar Gadaffi punde baada ya kuteuliwa siku ya Jumatatu.Kikao hicho kilianza Jumapili katika mji mkuu huo wa Ethiopia wakijumuika viongozi wa serikali na marais.


Viongozi hao wa mataifa 53 wanachama wa Umoja wa Afrika wanaripotiwa kuendelea na majadiliano hadi usiku hapo jana ila muafaka haukufikiwa.Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika Kanali Muammar Gaddaffi aliwasilisha pendekezo la kuunda shirikisho la mataifa ya bara la Afrika kwa lengo la kushajiisha maendeleo.Hata hivyo wazo hilo halikuungwa mkono na viongozi waliohudhuria kikao hicho.

Hali hiyo ya sintofahamu ilisababisha kurefushwa kwa kikao hicho kilichokua kimalizike hapo jana.

Viongozi hao kwa upande mmoja waliridhia kurefusha majukumu ya Kamisheni ya Umoja wa Afrika na pia kubadili jina lake na kuwa Mamlaka ya Umoja wa Afrika.Mabadiliko hayo yanaripotiwa kuzua mitazamo tofauti. Kwa mujibu wa Rais wa Afrika Kusini Kgalema Motlanthe mapendekezo ya kuimarisha Umoja wa Afrika yanahitaji kipindi cha miezi mitatu kutathmini utekelezaji wake.Kiongozi huyo aliyasema hayo alipohojiwa na shirika la habari la AFP pamoja na kituo cha televisheni ya kitaifa nchini mwake SABC.

Kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi anaripotiwa kuondoka kwenye meza ya mazungumzo bila ya kutoa kauli yoyote wakati mjadala huo ulipokuwa ukiendelea.


Mjumbe maalum wa Kanali Gaddafi katika Umoja wa Afrika Ahmed Gaddafaddad anasisitiza kuwa azma hiyo huenda ikatimia.''Bila shaka tumefurahishwa kuona kwamba wakazi wa bara la Afrika wanaweza kuwa na fikra za aina hiyo na kuwa na fikra za malengo ya baadaye.Bado mambo hayajakuwa ila tuko katika mkondo mmoja.Umoja wetu una jumla ya mataifa 53 au zaidi na tunataraji kuwa idadi hiyo itaongezeka na nina imani kuwa siku moja lengo letu la kuwa na shirikisho la mataifa ya bara la Afrika litatimia.''



Kanali Kaddafi amekuwa akitilia mkazo sio tu umuhimu wa kuimarisha sifa ya bara la Afrika katika jukwaa la kimataifa lakini pia kujipigia debe binafsi.Wazo la Shirikisho linapingwa na baadhi ya viongozi wa bara la Afrika ikitiliwa maanani namna alivyoingia madarakani miaka 40 iliyopita.Kiongozi huyo wa Libya aliingia madarakani kwa njia ya mapinduzi ya kijeshi na utawala wake wa kiimla umeshutumiwa na makundi mengi ya kutetea haki za binadamu.Kulingana na kiongozi huyo njia pekee ya kulisukuma mbele bara la Afrika linalozongwa na vita na ukame ni kuwa na shirikisho la bara zima.Mtazamo wa mataifa mengine kama vile Nigeria,Afrika Kusini,Ethiopia na Kenya ni kutimiza wazo hilo hatua kwa hatua.