1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sintofahamu yaendelea kugubika mazungumzo kuhusu Ukraine

Lilian Mtono
21 Januari 2022

Mazungumzo ya kidiplomasia kati ya Urusi na Marekani kuhusiana na mzozo wa Ukraine hayakufanikiwa kuibua suluhu ya msingi na sasa wanadiplomasia hao wanaangazia mazungumzo zaidi siku za usoni.

https://p.dw.com/p/45uu7
Blinken und Lawrow, Ukraine Gespräche in Genf
Picha: Pavel Bednyakov/Sputnik/picture alliance/dpa

Wanadiplomasia wawili wa ngazi za juu wa Marekani na Urusi wamehitimisha mazungumzo yao mjini Geneva huku waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken akisema ingawa yamekuwa ya wazi lakini hayakuwa na matokeo yoyote. Wanadiplomasi hao walikuwa wakijadiliana namna ya kupunguza hali ya mvutano kuelekea Ukraine, kukiwepo wasiwasi kwamba Urusi huenda ikaivamia Ukraine. 

Mawaziri hao wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken na Sergei Lavrov wa Urusi wamekutana katika wakati ambao Marekani unauona kama ni tete mno hasa kutokana na kitisho cha uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. 

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken ingawa alisema hawakutaraji kufikiwa chochote kikubwa kwenye mazungumzo hayo, lakini wanaamini wako katika njia nzuri zaidi ya kujua nafasi ya kila mmoja kwenye mzozo huo.

Amesema tu kwamba Marekani itaijibu Urusi kwa maandishi , wakati alipozungumzia matumaini ya hatua zaidi za kidiplomasiakatika kusuluhisha mzozo wa Ukraine baada ya mazungumzo hayo.

President Wilson Hotel, Genf
Mawaziri hao walikutana hapa kujadiliana kuhusu mzozo huo wa ukraine.Picha: Sergei Bobylev/TASS/picture alliance/dpa

Marekani na Urusi watajadiliana zaidi baada ya majibu ya Marekani.

Lakini hakufafanua iwapo majibu hayo ya kimaandishi yatakuwa ni kujibu mapendekezo ya kiusalama ya Urusi yaliyotolewa mwezi uliopita na Moscow, akisema Washingtton pia itajumuisha masuala yake. Blinken amesema anaamini kwamba wataweza kushirikishana na Urusi wasiwasi na mawazo yao kwa kina kimaandishi wiki ijayo na wamekubaliana kuyajadili kwa kirefu baada ya hapo.

"Sote tumejitoa kutumia diplomasia na mazungumzo kujaribu kutatua tofauti zetu. Ikiwa hilo haliwezekani na Urusi ikaamua kuendeleza uchokozi dhidi ya Ukraine, tutajibu mara moja kwa hatua kali. Ninachukua fursa hii kukushirikisha moja kwa moja maoni ya washirika wetu, pamoja na mawazo madhubuti ya kushughulikia baadhi ya maswala ambayo umeibua pamoja na wasiwasi mkubwa ambao wengi wetu tunao kuhusu hatua za Urusi.", alisema Blinken.

Lavrov aonya wadau kuacha kukurupuka.

Hata hivyo Blinken ameonya kutakuwa na ukomo wa kusonga mbele iwapo wanajeshi takriban laki moja wa Urusi wataendelea kukita kambi karibu na mpaka wa Ukraine, na kuongeza kuwa anapanga kukutana siku za usoni na Lavrov, huku akisita kuthibitisha kuhusu mkutano wa kilele kati ya rais Joe Biden wa Marekani na Vladimir Putin.

Soma Zaidi: Maoni: Putin atulia, huku magharibi wazunguka

NATO-Russland Rat tagt in Brüssel
Urusi inapingana na kujitanua kwa NATO katika eneo la mashariki.Picha: Alexey Vitvitsky/Sputnik/picture alliance/dpa

Lavrov kwa upande wake, alisema wamekuwa na mazungumzo ya kujenga na muhimu, na Marekani imekubali kujibu kwa maandishi matakwa yao kuhusu Ukraine na Jumuiya ya Kujihami, NATO wiki ijayo. Hatua hii inaweza kusogeza mbele angalau kwa siku chache uvamizi wa aina yoyote. Urusi haitaki Ukraine kukubaliwa uanachama wa NATO na inapingana na NATO kujitanua kwenye eneo la mashariki.

Alisema "Nilikwishasema kwamba tunasubiri jibu rasmi, kwa maandishi, kufuatia mapendekezo yetu. Baadaye, tutakutana tena. Kwa hivyo tusikurupuke. Rais Putin yuko tayari kila wakati kuwasiliana na rais Biden. Lakini mawasiliano kama haya lazima yaandaliwe kwa uangalifu, na lazima iwe wazi ni nini tutafikia kwa kutumia mamlaka ya viongozi wetu."

Aidha kwenye mazungumzo hayo, Blinken na Lavrov wameizungumzia Iran, wakisema muda wa kurejea kwenye makubaliano ya kuufufua mkataba wa nyuklia ni mdogo mno. Amesema makubaliano hayo ni mfano tosha kwamba Marekani inaweza kushirikiana na Urusi katika masuala ya kiusalama na kuiomba Urusi kutumia ushawishi na mahusiano yake naIran kuieleza kuhusu udharura wa mazungumzo hayo.

Mashirika: DPAE/AFPE/APE/RTRE