1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siri ya mafanikio ya Merkel

28 Agosti 2013

Angela Merkel ni nyota wa kisiasa. Licha ya kwamba huwa anavaa suti zenye rangi zinazofanya macho yote yaelekezwe kwake, Merkel ni mtu asiyependa kujionyesha sana mbele za watu.

https://p.dw.com/p/19OGd
Kansela Angela Merkel
Kansela Angela MerkelPicha: Reuters

Nyakati zimebadilika hapa Ujerumani. Utandawazi, ugaidi na mzozo wa sarafu ya Euro umewafanya watu wawe na hamu kubwa ya kupata usalama na mwongozo. Jambo hilo linaonekana vizuri kwa vijana, yaani watu waliokulia katika uongozi wa Kansela Angela Merkel. Wanasoshiolojia wanalielezea kundi hilo kuwa la watu ambao kwa kiasi fulani wanaweza kuelezewa kuwa wenye mitazamo ya kizamani na wasiothubutu. Ndoto yao ni kuanzisha familia, kuwa na ajira yenye uhakika na kumiliki nyumba.

Wanaomkosoa Merkel, ambaye amekuwa madarakani tangu 2005, wanasema, Merkel ndiye wa kulaumiwa kwa raia wa Ujerumani kujali mambo yao wenyewe bila kuwa na maono kwa ajili ya Ujerumani nzima. Kila mtu anajali maslahi yake na familia yake tu. Mtaalamu wa masuala ya siasa, Karl Rudolf Korte, haungi mkono wazo hilo mia kwa mia ila anasema ni kweli kwamba hata Merkel ni mtu asiyependa masuala yanayomhusu yeye kama mtu binafsi yatumike katika kampeni zinazoendelea. "Ni kwamba wakati huu amekubali watu wafanye kampeni kwa haiba yake, lakini kwa kweli hakuna jambo tunaloelezwa juu ya maisha yake binafsi. Na huu ndio utamaduni wa kizamani wa Wajerumani kwamba hatutaki kufahamu mambo ya siri ya mtu, bali kile tu anachokionyesha nje."

Mashabiki wa Merkel wakimpokea wakati wa kampeni
Mashabiki wa Merkel wakimpokea wakati wa kampeniPicha: Reuters

Ishara ya uimara

Picha ya Angela Merkel walionayo Wajerumani kichwani ni kama ngome wakati wa shida. Anakidhi matamanio ya Wajerumani ya kupata usalama na mwongozo kwa njia tofauti. Aliwaahidi wananchi wake kwamba Ujerumani itatoka na nguvu zaidi katika mzozo wa sarafu ya Euro. Na kweli: Taarifa za uchumi zimethibitisha hilo. Katika siasa za kimataifa anawapa watu hisia kuwa kwake, fedha ya Wajerumani iko katika mikono salama. Hata katika mwonekano wake wa nje, Merkel anatoa ishara ya uimara na kutokobadilika badilika.

Mtindo wake wa nywele hubadilika kwa mbali tu, anavaa nguo zinazofanana na hata anapozungumza hadharani daima anaonekana kuwa mtu halisi asiyejaribu kuiga mtu mwingine. "Anaonekana kama mtu asiyetaka kujionyesha," anasema Korte. "Ni mtu asiyecheka, daima yuko katika huduma kwa wapiga kura na si kwa ajili yake binafsi. Hivyo ndivyo watu wengi wanavyomchukulia."

Merkel habadiliki badiliki katika msimamo wala katika mtindo wa mavazi.
Merkel si mtu anayebadilika badilikaPicha: dapd

Ujanja wa kisiasa

Merkel mwenyewe amewahi kusema kuwa amejifunza kwa wazazi wake kutokuwa na papara, kuridhika na kazi na kuwa mtulivu. Mtaalamu wa siasa Karl-Rudolf Korte anaeleza kwamba kuzaliwa kwa Merkel katika familia ya mchungaji wa kiprotestanti kumechangia pia mafanikio ya Merkel. Kwa mtazamo wake, waprotestanti hutilia mkazo zaidi maisha ya kujishusha na ya wastani.

Ni ujuzi wake madarakani, ujanja wake wa kisiasa na uwezo wake wa kukabiliana na hali tofauti unaomfanya Merkel mwanasiasa mwenye mafanikio. Uwezo wake wa kuwa Kansela unatokana pia na ukweli kwamba ana mtazamo na mtindo wa maisha sawa na raia wengi.

Mwandishi: Kay-Alexander Scholz

Tafsiri: Elizabeth Shoo

Mhariri: Saumu Yusuf