1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sita wauawa katika shambulio dhidi ya mabasi Kenya

Admin.WagnerD1 Julai 2016

Watu sita wameuawa nchini Kenya baada ya washambuliaji wanaoshukiwa kuwa wa kundi la itikadi kali la Al-Shabaab kuyafyatulia risasi mabasi mawili kaskazini mashariki mwa nchi hiyo karibu na mpaka na Somalia.

https://p.dw.com/p/1JHJX
Kenia Tote bei Anschlag auf ein Dorf
Picha: Reuters/Stringer

Inspekta Jenerali mkuu wa Polisi IGP Joseph Boinnet, amesema maafisa wa jeshi hilo walioko kwenye eneo la tukio walikuta watu sita wakiwa wamepigwa risasi na kuuawa, na kuongeza kuwa msako dhidi ya magaidi hao ulikuwa unaendelea.

Boinnet alisema watu wengine wawili wamejeruhiwa, lakini mratibu wa usalama wa kanda ya Kaskazini-Mashariki Mohammed Saleh alisema watu wengi walijeruhiwa. Haikubainika bado iwapo wahanga wa shambulio hilo walikuwa raia au maafisa wa polisi waliokuwa wanatoa ulinzi katika mabasi hayo.

Shambulio hilo la Ijumaa asubuhi limetokea karibu na El Wak katika kaunti ya Mandera, eneo maskini la vijiji katika nchi hiyo ambako mashambulizi ya maafa sawa na hilo katika siku za nyuma yamedaiwa na kundi la Al-Shabaab lenye mafungamano na mtandao wa Al-Qaeda.

Ramani ya Kenya ikionesha eneo la Mandera, yalikotokea mashambulio ya sasa.
Ramani ya Kenya ikionesha eneo la Mandera, yalikotokea mashambulio ya sasa.

Kamishna wa kaunti ya Mandera Fredrick Shisia ameliambia shirika la habari la Reuters, kuwa shambulio hilo lilitokea majira ya saa tatu na nusu asubuhi ya Ijumaa, wakati mabasi hayo yakisafiri kwenda mjini Mandera kutoka mji mkuu Nairobi.

Mashambulio ya huko nyuma

Shambulio baya zaidi lilikuwa lile la Novemba 2014, wakati washambuliaji waliojihami kwa silaha walipolisimamisha basi na kuwatenganisha abiria kwa msingi wa dini na kisha kuwachinja wasio Waislamu 28. Shambulio sawa Desemba 2015 lilisababisha vifo vya watu watu, baada ya abiria Waislamu kuwakinga wenzao Wakristu.

Kundi la Al-Shabaab linapambana kuianguisha serikali inayoungwa mkono na jumuiya ya kimataifa mjini Mogadishu tangu mwaka 2007, lakini sasa limegeuzia mashambulizi yake dhidi ya Kenya, baada ya jeshi la nchi hiyo kutumwa nchini Somalia mwaka 2011 kupambana na waasi hao wa Kiislamu.

Tangu wakati huo Al-Shabaab imefanya mashambulizi ya mfululizo dhidi ya raia katika maeneo tofauti ya Kenya, likiwemo jengo la maduka mjini Nairobi, chuo kikuu cha Garrisa kaskazini-mashariki mwa nchi na vijiji vya pwani ya nchi hiyo.

Siku ya Alhamisi, wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani ilitoa onyo kwa raia wa nchi hiyo kuepuka kusafiri katika maeneo ya mipakani mwa Kenya kwa sababu ya vitisho vya kundi la Al-Shabaab, ambapo El Wak na Mandera ni miongoni mwa maeneo waliotahadharishwa kuyatemebelea.

Abiria wakikaguliwa na maafisa usalama kabla ya kupanda basi katika kaunti ya Mandera. Licha ya hatua kama hizo, washambuliaji bado wanafanikisha azma yao ya kuikosesha amani nchi hiyo.
Abiria wakikaguliwa na maafisa usalama kabla ya kupanda basi katika kaunti ya Mandera. Licha ya hatua kama hizo, washambuliaji bado wanafanikisha azma yao ya kuikosesha amani nchi hiyo.Picha: Reuters/G. Tomasevic

'Kenya iko salama'

Afisa mwandamizi katika wizara ya mambo ya ndani ya Kenya alisema onyo hilo halikuwa la haki kwa sababu ya kile alichodai kuwa usalama wa nchi hiyo ulikuwa umerejeshwa. Afisa huyo Karanja Kibicho, alisema Kenya iko salama, muda mfupi kabla ya habari za shambulio la sasa kujulikana.

Wiki iliyopita maafisa watano wa polisi waliuawa katika eneo hilo katika shambulizi ambalo pia kundi la Al-Shabaa lilinyooshewa kidole.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,rtre

Mhariri: Mohammed Khelef