1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SOFIA : Rais Bush yuko Bulgaria

11 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBsq

Rais George W. Bush wa Marekani amewasili katika mji mkuu wa Bulgaria Sofia.

Hicho ni kituo cha mwisho katika ziara yake ya hivi sasa barani Ulaya.Mazungumzo yake na viongozi wa Bulgaria yanatarajiwa kulenga juu ya mpango wa Marekani wa kuweka makombora ya kujihami barani Ulaya na hatima ya jimbo la Serbia la Kosovo.

Awali Rais Bush alifanya ziara fupi katika mji mkuu wa Albania Tirana ambapo alikutana na Waziri Mkuu Sali Berisha.Kufuatia mazungumzo yao Bush amesisitiza dai lake kwamba mpango wa Umoja wa Mataifa kuipatia uhuru Kosovo utekelezwe licha ya kupingwa na Serbia na Urusi.

Bush anasema anaunga mkono kwa nguvu mpango wa mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Martti Ahtisaari kuipatia uhuru Kosovo yenye waakazi wengi wa asili ya Albania na kwamba ametamka wazi mambo mawili moja ni kwamba kuendelea kuchukuwa hatua hiyo na pili ni matokeo ya mwisho ambayo ni uhuru.

Kwa mujibu wa Bush kile alichokisema kiko wazi kwa kila mtu kwamba matokeo yawe ni uhuru kwa hiyo mchakato huo usonge mbele.

Urusi imetishia kutumia kura yake ya turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuzuwiya azimio lolote lile ambalo linataka kuipatia uhuru Kosovo.