1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sokwe hatarini kutoweka kabisa duniani

P.Martin15 Aprili 2008

Nchini Kamerun walinzi wa viumbe asili wanapigania kuwa na mahala ambapo sokwe wa aina mbali mbali wataweza kuishi kwa usalama.

https://p.dw.com/p/DiWk
Der Gorilla Matze guckt am Donnerstag (06.12.2007) in seinem Gehege im Frankfurter Zoo zu den Besuchern. Der 1957 in Zentralafrika geborene Affe feierte seinen 50. Geburtstag. Der Silberrücken ist nach Angaben des Zoos der älteste Gorilla in der Zucht weltweit und hat bereits 17 Kinder gezeugt. Foto: Frank May dpa/lhe +++(c) dpa - Bildfunk+++
Sokwe-mtu Matze katika bustani ya wanyama pori (Zoo )mjini Frankfurt, Ujerumani alietimiza umri wa miaka 50 mwaka 2007.Picha: picture-alliance/ dpa

Kama kawaida adui wa wanyama hao ni binadamu.Mahala pekee pa usalama kwa sokwe hao,ni Bustani za Wanyama Pori.Sokwe,sawa na binadamu hutembea kwa miguu miwili,hula kila kitu na huweza pia kutumia baadhi ya vyombo vya mkono.Kwa maoni ya mlinzi mmojawapo katika bustani ya wanyama pori,kuwala wanyama waliofanana na binadamu ni sawa na kula nyama ya binadamu.Licha ya kuwa katika hatari ya kutoweka kabisa duniani,sokwe wanaendelea kuwindwa na nyama hiyo huuzwa sokoni na ukingoni mwa barabara.Sababu ni kuwa nyama hiyo ina faida kubwa kwani wengi huamini mtu anaekula nyama ya sokwe hupata nguvu za kiajabu. Joseph alie mlinzi katika Bustani ya Wanyama Pori ya Mfou kati kati ya Kamerun anasema:

"Hatuwezi kukanusha kuwa tunaishi katika jamii yenye mila na tamaduni zake.Kwa mfano kabila la Bakapimi kamwe halitokula nyama ya sokwe kwa sababu huamini kuwa hao ni binadamu walioadhibiwa na Miezi Mungu.Kwa hivyo imani hiyo inaweza kutumiwa kuhifadhi wanyama pori. Lakini kuna makabila mengine yanayoamini kuwa kwa kula nyama ya sokwe-mtu,watakuwa na afya na nguvu kama mnyama huyo."

Joseph akaongezea:

"Uwindaji haramu bado ni tatizo.Uwindaji wa aina hiyo husababisha watoto wa sokwe kuwa yatima na wanyama hao huletwa katika bustani yetu.Mara nyingine wanyama hao yatima huwekwa kama wanyama wa nyumbani licha ya kuwepo sheria zinazopiga marufuku kulea wanyama pori majumbani."

Kwa kweli Bustani ya Wanyama Pori kama hiyo,ingefaa kutumiwa kuwalea wanyama yatima na baadae kuwarejesha misituni wanyama hao walio katika hatari ya kutoweka humu duniani.Lakini Muingereza Ian Bickerstaff anaefanya utafiti wa wanyama wa hali ya juu katika Bustani ya Mfou nchini Kamerun ana wasi wasi wake. Anaeleza hivi:

"Kwanza ni kwamba Kamerun hakuna maeneo yenye ulinzi wa kutosha.Pili,ni kwamba sokwe wanaolelewa kwenye bustani za wanyama,hupoteza uoga wao wa asili.Kwa hivyo wanapokabiliana na binadamu misituni ni rahisi sana kuwa wahanga wa wawindaji haramu"

Tatizo lingine ni kuwa barani Afrika hakuna nchi inayoteketeza misitu yake bila ya kufikiria kama kunavyofanywa huko Kamerun.Malori husafirisha miti iliyokatwa hadi kwenye bandari ya Douala,kinyume kabisa na sheria.Lakini serikali huvumilia hayo kwa sababu biashara ya mbao huingiza pesa kwa mamilioni na wakati huo huo ardhi mpya hupatikana kupanda michikichi.Kwani hivi sasa kuna mahitaji makubwa ya mafuta ya chikichi katika nchi za Ulaya kuendeshea magari.

Mlinzi Joseph anasema,ingekuwepo njia nyingine ya kuingiza pesa Kamerun na wakati huo huo kuhifadhi misitu yake,basi hali ingekuwa bora.Lakini viwanda vya mbao vina usemi mkubwa mno.Kwa maoni yake,bila ya ushirikiano wa serikali,itakuwa vigumu kuhifadhi viumbe asili.Anasema,hakuna maana ya kuwalea wanyama yatima na hali wanaporejeshwa misituni huishia kuwa wahanga wa wawindaji haramu.Kilichokuwepo ni kutumaini kuwa siku moja Kamerun pia kama Ulaya itafanikiwa kuwarejesha tena misituni wanyama wanaolelewa katika Bustani za Wanyama Pori.