1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Solskjaer aleta ari mpya Manchester United

Bruce Amani
14 Januari 2019

Kurejea kwa Ole Gunnar Solskjaer katika klabu ya Manchester United kumeifufua tena hali ya mambo ndani nan je ya uwanja, lakini Mnorway huyo anasema kitu kinachoweza kumfanya aendelee kutabasamu ni kushinda mechi

https://p.dw.com/p/3BWWW
Manchester United-Trainer Ole Gunnar Solskjaer
Picha: Getty Images/C. Ivill

Solskjaer alifuzu mtihani wake mkali Zaidi akiwa kocha wakati timu yake iliifunga Tottenham Hotspur 1-0 katika Ligi ya Premier uwanjani Wembley kutokana na bao la Marcus Rashford na maajabu ya mlinda mlango David De Gea.

De Gea anasema kocha huyo wa muda, aliyechukua mikoba kutoka kwa Jose Mourinho aliyetimuliwa mwezi uliopita, amerejesha furaha katika klabu hiyo, lakini Solskjaer anaamini kuwa hali nzuri iliyoimarika inatokana na kinachofanyika uwanjani. "Ushindi huu ulikuwa mkubwa sana, shauku ya timu ilikuwa kubwa kabisa. Imani na furaha miongoni mwa wachezaji ni nzuri sana na bila shaka tumekuwa Dubai kwa wiki moja tukivifanyia kazi vitu kadhaa na wakati vijana wanapoona faida za kazi, kimwili na labda kimbinu, ni jambo kubwa na matokeo kama haya dhidi ya timu kubwa huwa yanakupa ujasiri.

Ushindi wa jana ulikuwa wa sita mfululizo tangu Solskjaer alipochukua usukani, na sasa wako katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi na pointi 41, nyuma ya Arsenal kutokana na tofauti ya mabao na pointi sita nyuma ya nambari nne Chelsea.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Iddi Ssessanga