1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Somalia-mazungumzo kuanza upya ?

19 Julai 2007

Mapigano makali yamekaribisha kuanza upya kwa mazungumzo ya kuleta muafaka nchini Somalia kati ya makundi mbali mbali.

https://p.dw.com/p/CB2h

Katika mkesha wa kuamkia kuanza upya kwa mazungumzo ya amani juu ya hatima ya Somalia, watu 4 wameuwawa.Miripuko mikubwa ilihanikiza leo katika soko la Bakara,mjini Mogadishu katika mapigano makali kabisa tangu siku 15 za machafuko mapya nchini Somalia.

Umoja wa Afrika uliamua jana kurefusha kwa miezi 6 mengine muda wa vikosi vyake vya kuhifadhi amani -hii ikiwa punde tu kabla muda huo kumalizika .Hadi sasa ni Uganda tu yenye vikosi nchini Somalia chini ya mpango huo.

Waasi walivifyatulia makombora ,mizinga na mabomu ya mkono vikosi vya serikali ya Somalia vilivyokuwa vikipiga doria katika soko la Bakara jana usiku.

Mashahidi wamearifu kuwa duka moja linalouza mafuta liliwaka moto pamoja na mengine sokoni.”Anga lilimurikwa na miripuko”-aliarifu mwenye duka la vyakula Mohamed Abdi.Haya ni mashambulio makubwa kabisa hadi sasa dhidi ya majeshi ya serikali ya Somalia.

Mkutano wa amani uliopangwa kuirejesha Somalia katika hali ya utulivu na kuponesha majaraha ya miaka 16,ulianza kwa muda mfupio tu jumapili na na mara ukaahirishwa baada ya hujuma za mizinga.

Hujuma hizi na vitisho zinatokana na kikundi cha Shabab-tawi la wakereketwa la Jumuiya ya kiislamu iliotawala sehemu kubwa ya Somalia kwa miezi 6 mwaka uliopita kabla kutimuliwa madarakani na majeshi ya Ethiopia yakiisaidia serikali kuu.

Katika kikao chake hapo jana, Baraza la amani na usalama la Umoja wa Afrika,lilitangazakurefusha muda wa vikosi vya kuhifadhi amani nchini Somalia ambavyo kwa sasa vimechangiwa na Uganda tu na muda wake takriban umemalizika. Vitabaki Somalia kwa kipindi kingine cha miezi 6.

Hapo kabla, kikosi cha hadi askari 8,000 kilipangwa kupelekwa Somalia mwanzoni mwa mwaka huu lakini, hadi sasa ni askari 1500 tu wote kutoka Uganda, ndio waliowasili Mogadishu ambako mara kwa mara wakishambuliwa.

Nigeria,Burundi,Malawi na Ghana zilizoahidi pia kuchangia majeshi,hazikutimiza ahadi zao hadi leo.Burundi ilitangaza wiki iliopita kuwa, kuchelewa kwa vikosi vyake kunatokana na ukosefu wa vifaa.

Wizara ya ulinzi ya Burundi imesema inasubiri kiasi cha dala 689,000 kutoka Ufaransa pamoja na sare,kofia za ngao na vizbao vya kujikinga na risasi kutoka Marekani pamoja na zana nyengine za kijeshi kutoka Kenya.

Katika mkutano wa kilele wa UA uliofanyika majuzi mjini Accra,Ghana, waziri mkuu wa Somalia Ali Mohammed Gedi, aliilaumu Jumuiya ya kimataifa kwa kutoiungamkono serikali yake na kuchelwewa kutumwa vikosi nchini mwake.

Jeshi la Uganda limesema liko tayari kubakia Somalia licha ya kuchelewa kwa nchi nyengine kuchangia majeshi yao.

Kurefushwa kwa muda wa kuweka vikosi vya kuhifadhi amani kumekuja siku moja kabla kurejewa mazungumzo ya amani ya kuleta suluhu baina ya vikundi mbali mbali vya wasomali na kuirejesha nchi hii ya Afrika mashariki katika hali ya utulivu.