1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Somalia:Wapiganaji wa Shebab wauteka mji wa Hodur

Miraji Othman/AFP25 Februari 2009

Somalia: mapigano moto mmoja

https://p.dw.com/p/H13k
Rais mpya wa Somalia, Sheikh Sharif AhmedPicha: ap

Wapiganaji wenye msimamo mkali wa Kiislamu huko Somalia leo waliuteka mji na kurejea kuushabulia mji mkuu wa Mogadishu, huku wakiendeleza hujuma zao dhidi ya rais mpya wa nchi hiyo, Sharif Sheikh Ahmed, na washirika wake. Si chini ya watu 17, wengi wao wakiwa wapiganaji, waliuwawa pale kikundi cha Shebab kilipoushambulia mji wa kaskazini magharibi wa Hodur na kuutwaa kutoka majeshi yanayoipendelea serekali.

Siku ya pili ya mapigano baina ya majeshi ya serekali na kikundi kingine cha wanamgambo wa Kiislamu katika mji mkuu wa Mogadishu pia ilisababisha vifo vyqa raia wanne. Wazee na mashahidi katika mji wa Hodur, mji mdogo ulio karibu na mpaka na Ethiopia, wanasema mapigano hayo yalikuwa makali na wakahakikisha kwamba wapiganaji wa Shebab wameuteka mji huo. Mzee wa mji huo, Adan Nur Mukhtar, amesema watu wengi walikufa katika mapigano hayo, na wamehesabu watu 14 waliokufa nje ya mji na watatu ndani ya mji. Pia kuna uwezekano wa kuweko maiti zaidi katika viunga vya mji huo. Mfanya kazi wa hospitali ya Hodur anasema idadi ya watu waliokufa kutoka jana asubuhi inatarajiwa kuzidi arbaini. Kamanda wa kikundi cha Shebab katika eneo hilo, Sheikh Hassan Derow, aliliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP, kwamba waliwauwa watu 20 na kuharibu magari mawili ya kivita. Alisema mji wa Hodur, ulio kilomita 300 kaskazini magharibi ya Mogadishu, sasa uko chini ya udhibiti wa kikundi chake cha Mujahidin.

Kikundi cha Shebab, ambacho zamani kilikuwa bawa la kijeshi la vuguvugu la Kiislamu katika nchi hiyo lililopinduliwa kutoka madarakani na majeshi ya Somalia yaliosaidiwa na REthiopia miaka miwili iliopita, kimefanya mashambulio kadhaa dhidi ya majeshi ya Ehiopia ambayo yaliondoka Somalia mwezi uliopita.

Katika miezi ya karibuni kikundi hicho cha Shebab kimeendesha operesheni dhidi ya makundi ya Kisomali yanayopingana na kuyateka maeneo makubwa ya nchi hiyo, hivyo kuyaacha majeshi ya serekali yanadhibiti vijieneo fulani katika mji mkuu wa Mogadishu.

Pia mapigano yalizuka tena mjini Mogadishu baina ya wanamgambo wa Kiislamu na majeshi ya serekali yanayosaidiwa na wanajeshi wa Umoja wa Afrika, AU. Raia wanne , akiwemo mtoto, waliuwawa kutokana na makombora ya mizinga ambayo yalizipiga nyumba na shule ya Quran katika mtaa wa Hodan, kusini mwa mji huo. Jana si chini ya watu 23 waliuwawa na zaidi ya 90 kujeruhiwa katika mapambano yaliotokea katika mji mkuu huo. Wapiganaji walio watiifu kwa Chama cha Hizbul Islamiya, yaani Chama cha Kiislamu, walidai dhamana ya mashambulio hayo ambayo yalizuka baada ya kuyashambulia majeshi ya serekali, kusini mwa Mogadishu. Chama hicho na kikundi cha Shebab vimezidisha hujuma zao dhidi ya serekali ya Sheikh Sharif, Muislamu mwenye siasa za wastani aliyechaguliwa kuwa rais wa Somalia, chini ya mapatano yaliosimamiwa na Umoja wa Mataifa.