1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SPD na mpango kabambe kwa wajerumani

3 Agosti 2009

Waziri Steinmeier aahidi mamilioni ya nafasi za ajira kufikia 2020,je ataweza?

https://p.dw.com/p/J2rq
Waziri wa mambo ya nje Frank Walter SteinmeierPicha: AP

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier mgombea wa chama cha SPD Social Demokratic Party ambaye atapambana na kansela Angela Merkel katika uchaguzi mkuu wa bunge mwezi ujao ameahidi kuunda mamilioni ya nafasi za kazi nchini Ujerumani.Lakini mambo hayaonekani yakuridhisha kwa upande wa waziri huyo wa mambo ya nje.Chama chake kiko nyuma ya chama cha CDU cha kansela Angela Merkel kwa asilimia 10 pamoja na chama ndugu cha CSU katika kura ya maoni.Hata hivyo katika harakati za kuimarisha kampeini yake Steinmeier leo anatangaza sera zake katika kile anachokiita mpango wa Ujerumani.akitangaza mapendekezo yake juu ya kuunda nafasi za kazi katika nishati sekta ya nishati endelevu,afya na viwandani.

Kwa mujibu wa manisfesto yake iliyochapishwa na gazeti la Der Spiegel Steinmeier amesema kwamba mpango wake kwa ujerumani utaweza kuunda jumla ya nafasi millioni 4 ya ajira mpya katika kipindi cha muongo mmoja ujao.Manisfesto hiyo ya kurasa 67 pia imetaja kwamba chama cha SPD kinataka kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira kufikia mwaka 2020 kama pia alivyosisitiza juu ya matumaini yao katibu mkuu wa chama hicho Hubertus Heil akisema

''Inawezekana kufikia lengo la kuongeza nafasi za ajira ikiwa tutaimarisha mifumo ya kijamii na pia tukiweza kuimarisha uzalishaji wa bidhaa mpya''

Mpango wa SPD kwa mujibu wa sera za Steinmeier ni kuimarisha sekta za nishati ambazo zinaweza kutoa mamilioni ya ajira pamoja na sekta ya viwanda vya kutengeneza magari ya kutumia umeme ambayo huenda yakatoa ajira kwa wajerumani millioni mbili.Takwimu kuhusu ukosefu wa ajira zilizotolewa wiki iliyopita nchini Ujerumani zilionyesha kwamba watu millioni 3.5 hawana ajira kufuatia mporomoko wa uchumi ulioikumba Ujerumani na idadi hiyo huenda ikaongezeka na kufikia watu millioni 4.5 kufikia katikati ya mwaka ujao kwa mujibu wa wanauchumi.Waziri wa uchumi Karl Theodor zu Guttenberg kutoka chama cha kihafidhina hata hivyo amemshutumu waziri Steinmeier akisema kwamba anatoa ahadi hewa.

Deutschland Tag der Deutschen Industrie 2009 Karl-Theodor zu Guttenberg
Waziri wa Uchumi Karl-Theodor Zu-Guttenberg asema SPD wanatoa porojo tu''Picha: AP

''Nafikiri watu katika nchi hii hawataki kusikia porojo zinazotolewa katika wakati wa kampeini za uchaguzi,na ikiwa mtu atazungumzia juu ya kufanya kitu hiki na kile kama kwa mfano kutoa mamilioni ya nafasi za kazi basi watu watatarajia hilo lifanyike''

Zu Guttenberg amesema kwamba wananchi wa Ujerumani wamechoka kusikia ahadi zinazotolewa wakati wa kampeini za uchaguzi na badala yake wanataka kuona mapendekezo maalum yatakayotoa matumaini.Serikali ya muungano ya Ujerumani inaongozwa na vyama ndugu vya CDU CSU pamoja na chama cha SPD hata hivyo vyama hivyo vimekuwa vikivutana mara zote katika kipindi cha miaka minne iliyopita.Kansela Angela Merkel na Steinmeier wote wameshazungumzia juu ya kutotaka kuwa na muunganao kama huo.

Chama cha CDU sasa kiko katika mapumziko ya msimu wa kiangazi kabla ya uchaguzi wa mwezi ujao lakini Steinmeier na chama chake cha SPD wako mbioni kukiimarisha chama chao pamoja na nafasi ya kiongozi huyo katika kuwania kuingia madarakani akiwa na mpango huo wa kuwapa nafasi za kazi wajerumani.Dirk Niebel katibu mkuu wa chama cha Free Demokratic FDP chama ambacho CDU cha Kansela Merkel kinatumai kuunda muungano pamoja nacho amemtaja Steinemeier kuwa ni mfa maji anayelazimika kutapatapa kutokana na chama chake kupoteza imani ya wajerumani waliowengi.Anasema SPD kinataka kufanya kila njia kurejesha imani ya wananchi.

►◄

Mwandishi Saumu Mwasimba

Mhariri Abdul-Rahman