1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SPD wataka makubaliano ya kuundwa seriklali yabadilishwe

Oumilkheir Hamidou
15 Januari 2018

Mada moja tu ndio iliyohodhi vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani asubuhi ya leo! Madai ya baadhi ya viongozi wa chama cha Social Democrat kutaka makubaliano yaliyofikiwa ijumaa iliyopita yafanyiwe marekebisho.

https://p.dw.com/p/2qqpF
Deutschland Abschluss der Sondierungen von Union und SPD
Picha: picture-alliance/Photoshot/S. Yuqi

Maoni ya wahariri yanalingana. Wanahisi wanasiasa wanalazimika kuweka wazi wanataka nini hasa. Gazeti la "Der neue Tag" linaandika: "Ni kichekesho kikubwa hiki kilichoshuhudiwa mwishoni mwa wiki. Hata saa 48 hazikufika baada ya makubaliano yaliyofikiwa kwa tabu na wawakilishi wa vyama ndugu vya CDU/CSU na wenzao wa SPD, sauti zimeanza kuhanikiza kutoka pande zote mbhili. Ndio, ni jukumu la waandishi habari kuuliza masuala na la wanasiasa kuyajibu masuala hayo. Wanasiasa lakini wanalazimika kupima wanachokisema, au kunyamaza kimya. Na kwa wakati huu tulio nao, muda mfupi kabla ya uamuzi kupitishwa na mkutano mkuu wa dharura wa SPD kama mazungumzo ya kuunda serikali yaanze, ingekuwa bora kunyamaza. Pupa za kuunda serikali ya muungano nchini Ujerumani zimechukua sura ya kiroja ambacho hakimchekeshi mtu yeyote. Pindi mwishoe uchaguzi mwengine ukibidi kuitishwa, jibu la wapiga kura linatarajiwa kuwa kali zaidi kuliko ilivyokuwa ikihofiwa."

SPD wanabidi wachague kati ya serikali na upinzani

Gazeti la "Landeszeitung linazungumzia changamoto zinazowakabili wana SPD wanaolazimika kuchagua kati ya kujiunga na serikali ya muungano wa vyama vikuu - "GroKo au kukalia viti vya upinzani au Opposition Mist," kama alivyosema wakati mmoja mwenyekiti wa zamani wa chama cha SPD, Franz Müntefering alipokuwa akizungumzia shida za kukalia viti vya upinzani. Gazeti hilo la mjini Lüneburg linaendelea kuandika: "SPD wanakabwa kwa mara nyengine tena na mtihani: Wanabidi wachague, wanataka kujiunga na serikali ya muungano wa vyama vikuu au wanataka kukalia viti vya upande wa upinzani. Wanabidi waamue kama wanataka kumdhoofisha mwenyekiti wao Martin Schulz au kumpa moyo. Jumapili inayokuja itajulikana wapi wanaelekea wana SPD. Ishara zimeshaanza kuchomoza. Katika jimbo la  Sachsen Anhalt, wajumbe wamepiga kura kwa wingi mdogo kupinga kuundwa serikali nyengine ya muungano wa vyama vikuu. Hata kama jimbo hilo linatuma wawakilishi 6 tu kati ya 600 watakaohudhuria katika mkutano mkuu jumapili inayokuja, hata hivyo matamshi yaliyotolewa na baadhi ya viigogo vya SPD mwishoni mwa wiki hayajamfurahisha Martin Schulz."

Vikwazo vya Umoja wa ulaya kwa uturuki vinaleta tija

Uhusiano kati ya Uturuki na Umoja wa Ulaya nao pia umezingatiwa. Gazeti la Berliner Zeitung linaandika: "Uturuki imeshaanza kuonja machungu ya vikwazo vya Umoja wa Ulaya, vikwazo vilivyopaliliwa zaidi na Ujerumani. Hakuna tena mikopo inayodhaminiwa na serikali kuu kwa mashirika yanayofanya biashara na Uturuki na hakuna tena mipango ya kupanuliwa umoja wa forodha. Msimamo huo mkali , viongozi nwa mjini Ankara hawakuufikiria. Na ndio maana rais Erdogan anaanza kubadilisha msimamo wake na kuanza kubembeleza akitaraji kufaidika na ukuaji wa kiuchumi nchini Ujerumani na katika Umoja wa ulaya. Ukweli ni kwamba Erdogan hana azma yoyote ya kurejesha mfumo wa nchi inayoheshimu sheria, kuliachia bunge lipitishe maamuzi wala kuanzisha mageuzi ya kidemokrasi.

 

Mandishi:Hamidou Oummilkheir/INlandspresse

Mhariri:Yusuf Saumu