1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SPD yaridhia mazungumzo na Merkel

21 Oktoba 2013

Viongozi wa chama cha Social Demokratik cha Ujerumani SPD leo Jumapili (20.10.2013) wamepata idhini kutoka chama chao kuanza mazungumzo na Kansela Angela Merkel ya kujiunga na serikali ya mseto kwa masharti.

https://p.dw.com/p/1A2s2
Mwenyekiti wa chama cha SPD Sigmar Gabriel katika mkutano wa chama Berlin (20.10.2013).
Mwenyekiti wa chama cha SPD Sigmar Gabriel katika mkutano wa chama Berlin (20.10.2013).Picha: Reuters

Viongozi wa chama hicho wameahidi kumshinikiza Merkel kuridhia madai yao wakati watakapoanza mazungumzo rasmi ya kujiunga na serikali ya mseto ikiwa ni pamoja na kima cha chini cha mshahara na usawa katika malipo.

Kwa mujibu wa waraka wa ndani iliouona shirika la habari la Uingereza Reuters Jumapili (20.10.2013),chama cha SPD kimesema madai yao 10 hayana mjadala ikiwa ni pamoja na kima cha chini cha mshahara cha euro nane na nusu kwa saa,malipo sawa kwa wanawake na wanaume, kuongeza uwekezaji katika sekta ya miundo mbinu na elimu na makakati wa pamoja wa kukuza uchumi na ajira wa kanda inayotumia sarafu ya euro barani Ulaya.

Waraka huo umeandaliwa na viongozi wa SPD kwa ajili ya mkutano wa Jumapili ambao kwayo wanachama waandamizi zaidi ya 200 wa chama hicho nchini kote wamepiga kura iwapo au la kuanza mazungumzo rasmi ya kuunda serikali ya mseto na wahafidhina wa Merkel.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa chama cha SPD Sigmar Gabriel kati ya jumla ya kura 229 zilizopigwa,kura 31 zilipinga na wajumbe wawili hawakushiriki kupiga kura.

Mwenyekiti wa chama cha SPD Sigmar Gabriel katika mkutano wa chama Berlin (20.10.2013).
Mwenyekiti wa chama cha SPD Sigmar Gabriel katika mkutano wa chama Berlin (20.10.2013).Picha: picture-alliance/dpa

Ameongeza kusema kwamba wanakusudia kuunda serikali hiyo kufikia Krismasi muda ambao unapaswa kuwa wa kutosha.

Madai mengine ya SPD

Chama hicho pia kitadai usawa wa malipo ya uzeeni kwa wastaafu katika ziliokuwa zikitambulika kama Ujerumani Mashariki na Ujerumani Magharibi ,kuwepo uwezekano wa kuwa na uraia wa nchi mbili na njia za kurahisisha maingiliano kati ya kazi na maisha ya kifamilia.

Suala la kuongeza kodi kwa matajiri halikutajwa ambalo SPD ililipigia debe wakati wa kampeni za uchaguzi kwa ajili ya uchaguzi wa mwezi wa Septemba lakini ambalo Kansela Merkel alilikataa.

Muungano wa kihafidhina wa Merkel wa chama chake cha Christian Demokratik Demokratik Union CDU na chama ndugu cha Christian Social Union CSU cha mkoa wa Bavaria viliibuka washindi katika uchaguzi wa Septemba 22 lakini vilishindwa kuunda serikali moja kwa moja kwa kutopata viti vya kutosha bungeni na ndio ikahitaji mshirika wa kuunda nao serikali ya mseto.

Chama cha SPD ambacho kilikuwa nyuma kidogo kwa kushika nafasi ya pili katika uchaguzi huo kuanzia mwanzo kilionekana kuwa yumkini ndio kikawa mshirika katika serikali mpya ya mseto lakini chama hicho kina shauku ya kuepuka marudio ya kuundwa kwa serikali ya muungano mkuu na Merkel kama ile ya mwaka 2005 hadi 2009.Matokeo yake yalisababisha kupata matokeo mabaya kabisa ya uchaguzi kuwahi kuyashuhudia tokea Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na kuwafanya wanachama wake wengi kuwa na mashaka kuhusu serikali ya muungano mwengine mkuu.

SPD kutimiza ahadi zake

Mwenyekiti wa chama cha SPD Sigmar Gabriel aliliambia gazeti la Ujerumani la Bild hapo Jumamosi kwamba safari hii anaweza kuhakikisha hawatokubali kuunda serikali ya mseto kwa kwenda kinyume na kile walichoahidi katika uchaguzi.

Erwin Sellering waziri mkuu wa jimbo la Mecklenburg- Vorpommern wa chama cha SPD amesema katika mahojiano na gazeti la Welt am Sonnntag hapo Jumapili kwamba Merkel anapaswa asifikirie kuwa kushinda katika uchaguzi kunamruhusu afanye kila anachotaka.

Erwin Sellering Waziri Mkuu wa jimbo la Mecklenburg-Vorpommern.
Erwin Sellering Waziri Mkuu wa jimbo la Mecklenburg-Vorpommern.Picha: picture-alliance/dpa

Amekaririwa akisema "Iwapo hatutoweza kushinikiza vya kutosha kile tulichoahidi,hapo itabidi tuwaambie wapiga kura :'samahani lakini hatupatikani' .......uchaguzi mpya sio kitu cha kufadhaisha kwetu."

Mazungumzo kati ya Merkel na chama cha mrego wa kati- kushoto cha SPD kuhusu sera za serikali hiyo ya mseto na nyadhifa za baraza la mawaziri yataanza Jumatano na yanaweza kuchukuwa mwezi mzima.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters

Mhariri: Grace Kabogo