1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sri Lanka yasema itawakomboa raia mnamo saa 48 zijazo

15 Mei 2009

Rais Mahinda Rajapaksa wa Sri Lanka ametangaza kuwa raia wote waliyonaswa katika eneo la mapigano kati ya serikali na waasi wa Tamil wataokolewa katika kipindi cha saa 48 zijazo.

https://p.dw.com/p/Hqrq
Mahinda Rajapakse Präsident Sri Lanka
Rais Mahinda Rajapakse wa Sri LankaPicha: AP

Kauli hiyo ya Rais Rajapaksa imekuja huku Shirika na Msalaba Mwekundu Duniani likisema kuwa hali wanayokabiliana nayo watu hao ni janga kubwa la kibinaadamu.


Rais Mahinda Rajapaksa alitangaza hayo mjini Amman Jordan jana usiku mbele ya wananchi wa Sri Lanka wanaoishi nchini Jordan.


Kauli hiyo ni kutia msisitizo wa uamuzi wa serikali yake kukataa wito wa jumuiya ya kimataifa kuitaka isitishe mashambulizi yake dhidi ya waasi hao wa Tamil Tigers kunusuru maisha ya maelfu ya raia waliyonaswa kwenye eneo dogo linalodhibitiwa na waasi.


Serikali inasema kuwa kiasi cha watu 20,000 wamenaswa kwenye eneo hilo , lakini mashirika ya Umoja wa Mataifa yanasema kuwa idadi hiyo inapindukia watu 50,000.


Jeshi la serikali linajiandaa kwa shambulizi la mwisho dhidi ya waasi hao wa Tamil Tigers, na mapema leo maelfu ya watu walifanikiwa kukimbilia kwenye maeneo ya pwani ya wilaya ya Mullaitivu ambayo iko chini ya udhibiti wa majeshi hayo.


Watu hao wametumia boti ndogo ya Shirika la Msalaba Mwekundu Duniani kunusuru maisha yao, lakini kutokana na idadi kuwa kubwa, wengine wameshindwa kukimbia.


Shirika la Msalaba mwekundu limekuwa likitumia boti hiyo kwa ajili ya kuwasaidia watu hao kama anavyothibitisha Bernard Barrett ambaye ni afisa wa shirika hilo.


Sri Lanka Bürgerkrieg Tamilen in Notunterkunft
Raia waliyojeruhiwa wakisubiri msaada katika eneo la Mullivaikal, Sri Lanka.Picha: AP

´´Tuna boti ambayo tumekuwa tukiitumia toka katikati ya mwezi February kuwaokoa watu ambao wamejeruhiwa vibaya au wagonjwa na pia kupeleka chakula kwa waliobaki. Mara ya mwisho kuitumia ilikuwa Jumamosi iliyopita. Mapigano yamekuwa makali sana toka wakati huo´´


Mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni ya serikali ya Sri Lanka anayeongozana na majeshi ya serikali, Saman Ramawickrema amesema ameona moshi mzito kwenye eneo linalodhibitiwa na waasi hao uliyosababishwa na mripuko mkubwa.


Anasema huenda waasi hao wameamua kulipua ghala la silaha zao nzito, na kuongeza kuwa kwa mujibu wa taarifa za idara ya ujasusi ya jeshi hilo, kiongozi wa kundi la Tamil Velupillai Prabhakaran pamoja na msaidizi wake Pottu Amman inaaminika bado wako kwenye eneo hilo.


Rais Barack Obama wa Marekani ameitaka serikali ya nchi hiyo kutotumia silaha nzito katika operesheni zake hizo kunusuru maisha ya raia.


Obama Chrysler
Rais Barack ObamaPicha: AP

´´Serikali ni lazima itimize ahadi yake ya kutotumia silaha nzito katika harakati zake na iruhusu wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada kwenda kwenye eneo la mapigano ili kuwapatia raia misaada muhimu kuokoa maisha yao´´


Hata hivyo serikali hiyo ya Sri Lanka imekataa kuruhusu wafanyakazi wa mashirika ya misaada kwenda kwenye eneo hilo ikisema kuwa haina uhakika na usalama wa maisha yao watakapokuwa huko.


Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amemtuma afisa mwandamizi wa umoja huo Vijay Nambiar kwenda nchini humo kujaribu kutafuta suluhisho la mzozo huo.


Mjini Washington, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton amelitaka Shirika la Fedha la Kimataifa IMF kutokubaliana na ombi la mkopo wa dola billioni 1.9 lililowasilishwa na serikali ya Sri Lanka.


Bibi Clinton amesema huu si wakati muafaka kwa serikali hiyo kupewa mkopo huo na IMF ambayo Marekani ina hisa kubwa katika shirika hilo.

Mwandishi:Aboubakary Liongo

Mhariri:Josephat Charo