1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

St. Petersburg yashambuliwa

Mohammed Khelef
3 Aprili 2017

Mji wa St. Petersburg umetikiswa kwa mripuko mkubwa kwenye kituo cha treni, ambao umeuwa watu 10 na kujeruhi wengine zaidi ya 20 wakati Rais Vladimir Putin akikutana na Rais Alexander Lukashenko wa Belarus.

https://p.dw.com/p/2aZzj
Russland Explosion Metro in Sankt Petersburg
Picha: Reuters/A. Vaganov

Kuna taarifa zinazopingana juu ya idadi ya miripuko, ambapo baadhi ya mashahidi wameliambia shirika la habari la Interfax kuwa ilikuwa miwili iliyotokea baina ya vituo viwili vya treni, huku wengine wakisema ulikuwa mmoja uliosababishwa na bomu lililokuwa na vitu vyenye ncha kali, wakati treni ikiwasili kituo cha Chuo cha Teknolojia kutoka kituo cha Sennaya.

Rais Putin ambaye alikuwa mjini humo wakati miripuko hiyo ikitokezea, aliwaambia waandishi wa habari mbele ya mgeni wake, Rais Lukashenko wa Belarus, kwamba uchunguzi unaendelea, lakini haondoshi uwezekano wa hayo kuwa mashambulizi ya kigaidi.

"Tutafanya kila kitu kujuwa sababu za kilichotokea, tutafanya uchunguzi wa kina na mamlaka za mji na serikali kuu zitafanya kila liwezekanalo kuzisaidia familia za waliouawa na raia waliojeruhiwa," alisema Putin.

Picha za televisheni zimewaonesha watu wakiwa wamelala sakafuni wakivuja damu, huku wengine wakitibiwa na mashirika ya huduma za dharura, na wengine wakikimbia kwenye eneo la tukio wakati moshi mkubwa ukitanda.

Behewa moja linaonekana likiwa na tundu kubwa, huku abiria wakikimbilia kutoka nje kupitia viyoo vilivyopasuka. 

Ulinzi waimarishwa Moscow na St. Petersburg

Vituo vyote vya usafiri wa treni wa chini ya ardhi vimezuiwa kufanya kazi zake, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali, ambavyo pia vimeinukulu Kamati ya Kupambana na Ugaidi ya Urusi ikisema kuwa ulinzi umeimarishwa kwenye miundombinu yote ya usafiri sio tu kwenye mji wa St. Petersburg, bali hata mji mkuu, Moscow.

Russland Präsident Putin in Sankt Petersburg
Rais Vladimir Putin wa Urusi anasema hapuuzii uwezekano wa kuwa haya yalikuwa mashambulizi ya kigaidi.Picha: picture-alliance/dpa/M. Metzel

Mkuu wa kitengo cha habari kwenye ofisi ya gavana wa St. Petersburg, Andrey Kibitov, ameandika kwenye akaunti yake ya Twitter kwamba watu waliojeruhiwa kwenye mripuko huo hadi sasa ni 50, huku magari ya kuhudumia wagonjwa yakiendelea kutoa huduma ya kwanza kwa manusura. 

Urusi imekuwa ikiandamwa na mashambulizi kutoka kwa wanamgambo wa Chechenya. Mnamo mwaka 2010, washambuliaji wawili wa kike walijiripua katika kituo cha treni kilichojaa watu mjini Moscow na kuuwa watu 38. 

Mwaka 2004, watu 330, nusu yao watoto wadogo, waliuawa baada ya polisi kuivamia skuli moja kusini mwa Urusi, ambayo ilitekwa na wapiganaji wa Kiislamu. 

Mwaka 2002, mateka 120 waliuawa wakati polisi kwa mara nyengine tena walipolivamia jumba la maonyesho mjini Moscow, ili kuumaliza utekaji nyara mwengine.

Akiwa waziri mkuu mwaka 1999, Putin alianzisha operesheni ya kuiandama serikali ya Chechenya ambayo ilikuwa ikipigania kujitenga kwa jimbo hilo lenye Waislamu wengi kusini mwa Urusi, na ameendelea kuwa na msimamo mkali dhidi ya waasi wa huko hadi sasa akiwa rais.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/afp
Mhariri: Iddi Ssessanga