1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinbrueck apongeza kuungana kwa benki mbili za Ujerumani

Charo, Josephat1 Septemba 2008

Hisa zashuka kwenye soko la hisa la Frankfurt na nafasi 9,000 za ajira kupunguzwa

https://p.dw.com/p/F8nl
Waziri wa fedha wa Ujerumani Peer StreinbrueckPicha: AP

Kumezuka hisia tofauti kufuatia kuungana kwa benki za Ujerumani za Commerzbank na Dresdner. Hisa za benki ya Commerzbank zimeshuka kwa kiwango kikubwa hii leo huku serikali ikiahidi kuimarisha sekta ya benki humu nchini.

Masoko ya hisa ya hapa Ujerumani yameathiriwa na hatua ya benki ya Commerzbank na Dresdner kuungana. Hisa za Commerzbank zimeshuka kwa asilimia 11 hii leo katika soko la hisa la mjini Frankfurt. Kielelezo cha hisa za DAX kimeshuka kwa asilimia 0.75.

Gazeti la Financial Times Deutshland limesema katika taarifa yake ya leo kwamba hii inadhihirisha mambo matatu; kwanza benki ya Commerzbank haina opesa za kutosha kuinunua benki ya Dresdner. Hii ni hatari. Pili kampuni ya bima ya Allianz inayoimiliki benki ya Dresdner haiwezi kulitatua tatizo lake, hizo ni habari mbaya kwa wenye hisa. Na hatimaye pande zote husika katika makubaliano hayo hazijafurahia mkataba uliosainiwa.

Martin Blessing, meneja wa benki ya Commerzbank aliyechukua nafasi hiyo miezi mitatu iliyopita anasema, ´´Hatua ya kuichukua benki ya Dresdner kutaifanya benki ya Commerzbank kuwa taasisi imara´´.

Waziri wa fedha wa Ujerumani Peer Steinbrueck hii leo amesema hatua ya benki ya Commerzbank kuinunua benki ya Dresdner huku kukiwa na ushindani mkubwa kutoka kwa benki moja ya China, itakuwa ya manufaa makubwa kwa Ujerumani. Katika taarifa yake aliyoitoa akwia mjini Beijing nchini China, Steinbrueck amesema hatua hiyo ni nzuri kwa Ujerumani kama kituo cha shughuli za kifedha na inakiimarisha kituo hicho.

Naibu waziri wa fedha Joerg Asmussen amesema serikali ya Ujerumani haikutumia ushawishi wowote wa kisiasa kuhusiana na kuuzwa kwa benki ya Dresdner kwa benki ya Commerzbank kwa kiasi cha euro bilioni 9.8. Benki ya Commerzbank ilikabiliwa na ushindani mkubwa kutoka kwa benki ya maendeleo ya China iliyotaka pia kuinunua benki ya Dresdner. Naibu waziri wa fedha Joerg Assmussen amesisitza kwamba uamuzi huo ulifikiwa na wamilikaji hisa wa benki ya Commerzbank na kampuni ya bima ya Allianz.

Steinbrueck na Asmussen wamefanya mazungumzo na maafisa wa China akiwemo naibu waziri mkuu Li Keqiang, waziri wa fedha Xie Xuren na gavana wa benki kuu ya China, Zhou Xiaochuan mjini Beijing.

Lakini hata hivyo ndoa kati ya benki hizo itasababisha nafasi za ajira 9,000 kutoka kwa idadi ya wafanyakazi wake jumla ya 67,000. Nafasi 2,500 za ajira zitapunguzwa katika matawi ya muungano huo yaliyo kwenye nchi za kigeni.

Uwe Foullong wa chama cha wafanyakazi cha Verdi hapa Ujerumani anasema wamekuwa wakipinga kuungana kwa benki ya Commerzbank na benki ya Dresdner

´´ Kila mara tumekuwa tukionya kuhusu muungano huu mkubwa kwa kuwa unahatarisha maelfu ya nafasi za ajira na sasa tumeweza kushuhudia ukweli huo´´.

Benki ya Commerzbank na kampuni ya bima ya Allianz zilitangaza makubaliano yaliyofikiwa na bodi zinazosimamia benki hizo kutiliana saini kuziunganisha baada ya mikutano tofauti kati ya bodi hizo iliyofanyika jana Jumapili.

Benki ya Commerzbank inashikilia nafasi ya pili kwa ukubwa hapa Ujerumani huku benki ya Dresdner ikishikilia nafasi ya tatu. Benki ya Deutsche Bank iliyoshindwa kuungana na benki ya Dresdner miaka minane iliyopita bado inashikilia nafasi ya kwanza ikiwa na mali ya thamani ya euro trilioni mbili.

Ukiwa na mali ya thamani ya euro trilioni 1.09 na wateja milioni 11 wa kijerumani, muungano mpya wa benki ya Commerzbank na Dresdner utasababisha kuchipuka kwa benki mpya iliyo imara zaidi katika taifa linaloongoza kihcumi barani Ulaya.

Lakini hata hivyo ndoa kati ya benki hizo itasababisha nafasi za ajira kupunguzwa kwa 9,000 kutoka kwa idadi ya wafanyakazi wake jumla ya 67,000. Nafasi 2,500 za ajira zitapunguzwa katika matawi ya muungano huo yaliyo kwene nchi za kigeni.