1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeier ataka uhuru, udhibiti wa intaneti

1 Julai 2014

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, amesema muda umefika kwa dunia kuwa na sheria za kimataifa zinazolinda uhuru wa mitandao ya intaneti na pia zinazohakikisha ulinzi wa taarifa za faragha.

https://p.dw.com/p/1CTgY
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, akihutubia Kongamano la Kimataifa la Vyombo vya Habari, tarehe 1 Julai 2014.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, akihutubia Kongamano la Kimataifa la Vyombo vya Habari, tarehe 1 Julai 2014.Picha: DW/M. Müller

Steinmeier ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza kwenye Kongamano la Kimataifa la Vyombo vya Habari linaloendelea kwa siku ya pili hapa Bonn, huku kiwango cha imani kati ya Ujerumani na Marekani kikishuka, kutokana na udukuzi wa Shirika la Usalama la Marekani (NSA) kwa taasisi na viongozi wa serikali barani Ulaya.

Steinmeier ametumia hotuba yake mbele ya wajumbe zaidi ya 2,000 sio tu kuzungumzia changamoto za vyombo vya habari duniani, bali pia sera ya nje ya Ujerumani kuelekea mawasiliano ya mitandaoni. Amewaambia washiriki hao kwamba bado mawasiliano ya mtandao wa intaneti yana changamoto kubwa, na hivyo yana umuhimu wa pekee kwenye kwenye sera ya nje ya Ujerumani.

Hata hivyo, Steinmeier amesisitiza kuwa licha ya kuwa sera za nje za mataifa zinahusu pia uzuwiaji wa baadhi ya mambo yake yasiwe hadharani, ukweli kuhusu mawasiliano ya mitandao unaondosha vizuizi hivyo.

"Sababu nyengine ni kwamba uhodari wa sera ya nje kuwa kwenye dola unayoweza kudhibiti data ambazo zimo kwenye mikono binafsi. Yote haya yanahitaji kanuni za pamoja za mitandao duniani, na hivyo mdahalo wa kiwango cha juu unahitajika, kwanza juu ya uhuru wa intaneti, lakini kwa upande mwengine juu ya ulinzi wa mambo ya faragha chini ya sheria za kimataifa.”

Marekani na Ujerumani kwenye mitandao

Ni baina ya masuala hayo muhimu kwenye ulimwengu wa sasa wa kimawasiliano, ndipo washirika wakubwa kimataifa, Ujerumani na Marekani, wanapojikuta sasa wakipoteza imani baina yao, katika kiwango cha kutia mashaka uhusiano wa muda mrefu kati yao.

Waziri wa Mambo wa Nje wa Marekani, John Kerry (kushoto) na mwenzake wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier.
Waziri wa Mambo wa Nje wa Marekani, John Kerry (kushoto) na mwenzake wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier.Picha: picture-alliance/dpa

“Marafiki zangu wengi ambao wameyajua mahusiano ya kati ya Ulaya na Marekani kwa miongo mingi sasa, wana wasiwasi kwamba hisia za kuichukia Marekani zinakuwa kwenye nchi hii, ambazo sio tu zinachochewa na siasa za mrengo wa shoto, na nadhani ni vigumu kuijenga ile hali ya kuaminiana na kama alivyosema Steinmeier, tunapaswa kutumia njia zote za majadiliano kujenga imani hiyo, kwani ikikosekana hakutakuwa na ushirikiano kati ya pande hizi,” amesema Rüdiger Lentz, mkurugenzi wa Taasisi ya Aspen ya Ujerumani, ambaye amefuatilia hotuba ya leo ya Steinmeier kwenye kongamano hilo.

Mwanzoni mwa mwaka huu, mvujishaji siri wa Marekani, Edward Snowden, ambaye kwa sasa ameomba hifadhi nchini Urusi, alisema kwamba NSA ilikuwa likitega simu ya mkononi ya Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.

Mbali na hotuba hiyo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, kongamano liliendelea hadi jioni ya leo, huku washiriki wakijadilia nafasi ya mitandao ya kijamii kwenye mabadiliko ya fikra barani Afrika, na pia ubunifu na ushiriki wa vijana kwenye mawasiliano ya kisasa, miongoni mwa mada nyengine kadhaa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DW Kiswahili
Mhariri: Yusuf Saumu