1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeier azitembelea nchi tatu za Afrika Magharibi

11 Februari 2008
https://p.dw.com/p/D5fa

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeir, anafanya ziara ya siku tatu barani Afrika.

Akianza ziara hiyo hapo jana waziri Steinmeier aliahidi kwamba Ujerumani itazisaidia juhudi za katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, kujaribu kuutanzua mgogoro wa kisiasa nchini Kenya.

Steinmeier aliwasili jana mjini Accra, Ghana ambako alifanya mazungumzo na mwenzake wa nchi hiyo, Akwasi Osei Adjei.

Steinmeier amesema naibu waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani, Gernot Erler, yuko nchini Kenya kumsaidia Kofi Annan kutafuta suluhisho la mzozo wa kisiasa kati ya serikali na upinzani uliozuka baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa mwezi Disemba mwaka jana.

Erler atashiriki katika mazungumzo ya leo kati ya wajumbe wa upinzani na serikali katika hoteli moja mjini Nairobi.

Waziri Steinmeier anatarajiwa kwenda nchini Togo hii leo ambako anatarajiwa kukifungua rasmi kituo cha matibabu ya magonjwa ya nchi za joto.

Hapo kesho atakamilisha ziara yake nchini Burkina Faso, ziara ambayo ni ya pili katika eneo la Afrika Magharibi katika kipindi cha miezi saba.