1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeier kuwa mgombea ukansela wa SPD uchaguzi mkuu ujao

Abdulrahman, Mohamed8 Septemba 2008
https://p.dw.com/p/FDNR
Bw Frank Walter-Steinmeier .Picha: AP

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier kutoka chama cha Social Democrats-SPD, ameteuliwa na chama chake kuchuana na Kansela Angela Merkel wa chama cha Christian Democrats-CDU, katika uchaguzi mkuu mwaka ujao 2009. CDU na SPD kwa sasa vinaunda serikali ya mseto mjini Berlin. Kuteuliwa Bw Stenmeier kumekuja katika wakati ambao umaarufu wa SPD miongoni mwa wapiga kura unazidi kupungua.

Katika hatua ya kushangaza Mwenyekiti wa zamani wa chama hicho cha SPD Franz Muentefering mwenye umri wa miaka 68, alirudi tena baada ya kupumzika siasa kumuuguza mkewe na kushika tena wadhifa wa Mwenyekiti kutoka kwa Kurt Beck aliyetangaza kujiuzulu katika wadhifa huo.

Akizungumza baada ya kuteuliwa Steinmeier alisema,"Kampeni ya uchaguzi haianzi leo, lakini tayari tumo mchezoni kuelekea uchaguzi wa Shirikisho 2009." Steinmeier akaongeza,"Kurt Beck alieleza wazi katika kikao , kwamba kwake yeye ni jambo lililokua likifahamika kwa miezi kadhaa kuwa mimi niwe mgombea wa Ukansela. Nilizungumza naye sula hilo muda mrefu katika hali ya kuaminiana. Tuliafikiana kuwa sasa ni wakati muwafaka wa kufikia maamuzi."

Mwenyekiti anayeongoka Kurt Beck amekua akilaumiwa kwa kushuka kwa umaarrufu wa chama hicho miongoni mwa wapiga kura, kwa kile wengi walichokiona kuwa ni kukiuka ahadi za chama.

Mabadiliko hayo yaliokubaliwa na kamati kuu ya chama katika mkutano wake Schwielowsee kilomita 25 kutoka mji mkuu Berlina pia yamewarudisha wanamageuzi. Wote wawili Steinmeier na Muentefering ni watetezi wa mageuzi ya kiuchumi yaliopwewa msukumo na Kansela wa zamani kutoka SPD Gerhard Schröder, ambayo yalisababisha wafuasi wengi wa jadi wa chama hicho kuanza kukipa mgongo. Wakati uamuzi huo umekuja mapema kuliko ilivyotarajiwa, wadadisi wengi wanaashiria kwamba ushirika wa watu hao wawili utafanya kazi.

Muentefering anatazamwa na wengi kuwa ni mtu mwenye uwezo wa kuleta umoja chamani na anaweza kuwarudisha wafuasi wa bawa la shoto licha ya kwamba binafsi anatetea mageuzi. Aliwahi kuzusha dharuba 2005 alipowafananisha wawekezaji fedha kuwa sawa na "nzige", matamshi ambayo yalionekana kuwapendeza wachama wakereketwa wa SPD.

Mtihani mkubwa kwa SPD umekua ni wanachama wake kukigeukia chama cha mrengo wa shoto Linke kinachoongozwa na Mwenyekiti wa zamani wa SPD Oskar Lafontaine, ambaye aliihama SPD baada ya kutafautiana na Bw Schröder juu ya mageuzi, huku vigogo wakimtaja kuwa ni msaliti.

Bw Steinmeier mwenye umri wa miaka 52 alikua mnadhimu mkuu katika Ofisi ya Kansela Schröder kabla kuwa Waziri wa mambo ya nchi za nje miaka mitatu iliopita. Anatajwa kuwa ni mpangaji mzuri wa mambo na baadhi ya kura za maoni zinaonyesha ni mwanasiasa maarufu nchini Ujerumani wakati huu. Lakini hakupata kuchaguliwa kushika wadhifa wowote kisiasa na kuna shaka shaka vipi ataibuka kuwa kivutio .

Kura za maoni ya wapiga kura za stesheni ya matangazo ya ARD ilionyesha uungaji mkono kwa SPD umeshuka hadi 26 asili mia ikiwa ni pointi 10 nyuma ya kambi ya wahafidhina ya Kansela Merkel.