1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Stoltenberg akutana na Trump

Lilian Mtono
3 Aprili 2019

Katibu mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg amekutana na kufanya mazungumzo na rais Donald Trump wa Marekani katika ikulu ya White House wakati jumuiya hiyo ikijiandaa kwa maadhimisho ya miaka 70.

https://p.dw.com/p/3G7m5
US Präsident Trump und NATO Generalsekretär Stoltenberg
Picha: Reuters/J. Roberts

Hata hivyo rais Trump kwa mara ya kwanza amekiri kwenye mazungumzo hayo kwamba mataifa wanachama wa NATO yamejiimarisha katika suala la michango, lakini akisema anatarajia kuona yanajiimarisha zaidi.

Trump alisifu ushirikiano baina yake na Stolteberg katika kuhakikisha mataifa hayo wanachama yanatoa michango yao, lakini pia akiuita uhusiano baina yao kuwa ni "mzuri sana".

Donald Trump NATO Conference
Rais Donald Trump alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kukutana na katibu mkuu wa NATO, Jens StoltebergPicha: picture-alliance/NurPhoto/J. Arriens

Trump mara kwa mara alilalamika kwamba Marekani inabeba mzigo mkubwa wa ufadhili kwenye ushirika huo wa kijeshi, huku akiitaja Ujerumani, wakati akijibu swali kutoka kwa mwandishi wa DW mjini Washington Alexandra von Nahmen aliyemuuliza kuhusu mchango wa Ujerumani.

Alisema ni kweli kwamba Ujerumani haitoi mchango wake kihalali, na kuongeza kuwa haitoi kiwango inachopaswa kutoa, wanatoa karibu asilimia 1 tu. Trump alisema anataka kuona wanachama wa NATO wanalipa zaidi ya asilimia 2 ya pato la ndani la taifa, GDP kwa ajili ya ulinzi.

Alilalama kwamba Marekani inalipia mataifa mengine kwa ajili ya kuwalinda watu wao.

Katibu mkuu wa NATO, Stoltenberg alirejelea matamshi hayo ya Trump akisema ana matarajio kwamba Ujerumani itaanza kuchangia ahadi aliyokubaliana na washirika wenzake wa NATO. 

Eröffnungsfeier Hannover Messe 2019
​Ujerumani inalaumiwa kwa kushindwa kuchangia sawa na ahadi yake kwenye NATOPicha: picture-alliance/dpa/F. Gentsch

Stoltenberg, alisema kabla ya kuondoka Brussels kuelekea Washington kwamba anataraji Ujerumani itafikia kiwango cha ahadi yake ya ulinzi, na kuongeza kuwa ilikwishawasilisha mkakati wa kitaifa ambao walieleza kwa kina namna itakavyoongeza bajeti yake kwenye masuala ya ulinzi hadi asilimia 80 katika kipindi cha miaka 10.

Mchango wa Ujerumani ulianza kutupiwa jicho tangu rais Donald Trump alipoingia madarakani miaka miwili iliyopita. Aidha, Trump ametishia kuiondoa Marekani kwenye Jumuiya hiyo ya NATO, iwapo mataifa wanachama hayataongeza kiwango cha michango yao ya ulinzi.

Ziara katika ikulu ya Marekani, inafanyika siku mbili kabla ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa NATO mjini Washington ambapo suala la Urusi linatarajiwa kuibuka upya. Hatua zinazofuata baada ya kuvunjika kwa makubaliano ya kimataifa yanayopiga marufuku makombora ya nuklia ya masafa marefu pia yatajadiliwa wakati wa mkutano wa siku mbili wa mawaziri wa mambo ya nchi za nje katika kuadhimisha miaka 70 ya tangu NATO ilipoundwa.

Mwandishi: Lilian Mtono/DW

Mhariri: