1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan Kusini yawaingiza watoto jeshini - Umoja wa Mataifa

Mohammed Khelef19 Agosti 2016

Waraka uliotolewa na Umoja wa Mataifa unaishutumu serikali ya Sudan Kusini kuwapa mafunzo ya kijeshi watoto wadogo wiki iliyopita, ikijitayarisha kwa uwezekano wa mapigano mapya.

https://p.dw.com/p/1JlLV
Wanajeshi wa Sudan Kusini.
Wanajeshi wa Sudan Kusini.Picha: Reuters

Waraka, ambao shirika la habari la Associated Press limeupata, unasema kuwa mwanasiasa mmoja wa ngazi za juu aliyeteuliwa na Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini ndiye aliyeongoza mafunzo hayo ya kijeshi kwa wavulana wa kijiji kizima, huku akitumia vitisho, kwa wale wanaokataa. Kwa mujibu wa waraka huo, miongoni mwa wavulana hao walioorodheshwa kujiunga na mapigano, wamo wenye umri wa hadi miaka 12.

Hata hivyo, msemaji wa jeshi la serikali, Lul Ruai Koang, amekanusha taarifa hizo, na badala yake akasema vijana wote wanaojiunga na jeshi huwa hawalazimishwi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizomo kwenye waraka huo, uingizaji wa watoto jeshini ulianza muda mchache baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio la kutuma wanajeshi wengine 4,000 wa kulinda amani katika taifa hilo la Afrika Mashariki, ili kuwalinda raia, kufuatia kuanza upya kwa mapigano katika mji mkuu, Juba, mwezi uliopita.

Tabia ya makundi hasimu kutumia watoto kama wapiganaji kwenye mapambano yao, imekuwepo kwa muda mrefu kwenye taifa hilo jipya kabisa barani Afrika.

Umoja wa Mataifa unasema watoto 650 wamejiunga na makundi yenye silaha nchini Sudan Kusini mwaka huu pekee. Kiasi cha watoto 16,000 wameingizwa kwenye makundi hayo tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe kuanza Disemba mwaka 2013.

Riek Machar yuko DRC

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umethibitisha ushiriki wake katika kumsafirisha kiongozi wa zamani wa waasi, Riek Machar, ambaye kwa sasa amekimbilia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kiongozi wa chama cha SPLM, Riek Machar, ambaye amekimbilia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kiongozi wa chama cha SPLM, Riek Machar, ambaye amekimbilia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Picha: picture-alliance/dpa/Stringer

Msemaji wa Umoja huo, Farhan Haq, amesema kuwa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja huo nchini Kongo, MINUSCO, kilihusika na operesheni hiyo, kwa idhini na mashirikiano ya serikali ya Kongo.

"Tunaweza kuthibitisha kwamba operesheni hiyo ilifanywa na MONUSCO kwa misingi ya kibinaadamu ili kuwezesha kumsafirisha Riek Machar, mkewe na wengine kumi kutoka eneo fulani nchini Kongo, kwa msaada wa mamlaka za Kongo. Na kama ambavyo nimesema, ameshakabidhishwa kwa mamlaka za Kongo na yuko nao sasa." Alisema Haq.

Jana chama cha Machar kilithibitisha kuwa kiongozi wao huyo ametoroka nchi hiyo, kikisema amekimbilia nchi jirani kwa usalama wake.

Machar, ambaye alirejea kwenye nafasi yake ya umakamu wa rais chini ya makubaliano ya amani ya mwaka 2015, alilazimika kuondoka mjini Juba akiambatana na wanajeshi wake mwezi uliopita, baada ya kuzuka upya kwa mapigano kati ya vikosi vyake na vile vya Rais Kiir.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga