1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan yaipelekea Israel Baraza la Usalama

25 Oktoba 2012

Sudan imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liilaani Israel kwa kukishambulia kiwanda chake cha silaha mjini Khartoum, ikisema kwamba ina ushahidi kuwa mashambuizi hayo yalifanywa na ndege za Israel.

https://p.dw.com/p/16WYY
Kiwanda cha silaha cha Yarmouk kikiwaka moto baada ya mashambulizi.
Kiwanda cha silaha cha Yarmouk kikiwaka moto baada ya mashambulizi.Picha: Reuters

Waziri wa Habari na Utamaduni wa Sudan, Ahmed Bilal Osman, ameeleza kuwa ndege nne za Israel zilizoweza kuikwepa rada ya Sudan zilifanya mashambulizi hayo kwenye kiwanda cha silaha cha Yarmouk kusini mwa mji wa Khartoum.

Sudan inadai kwamba mwaka mmoja na nusu uliopita Israel pia ilifanya mashambulizi kama hayo. Osman sasa anatishia kulipiza kisasi.

"Tunapaswa kujibu, kwa sababu mambo yamezidi.Hii ni mara ya nne kwamba Israel imetushambulia.Tunayo haki ya kuzishambulia sehemu zenye maslahi ya Israel popote pale. Ni wazi kwamba hatutaishmbulia Israel, lakini tunao uwezo. Tunao uwezo wa namna ya kujibu mashambulio. Israel imewaua watu wetu.Uhai wa watu hao pia una thamani. Tunajua namna ya kulipiza kisasi." Amesema Osman.

Watu wanaoishi karibu na kiwanda cha silaha cha Yarmouk wemeliambia shirika la habari la AFP kuwa waliona jinsi ndege au kombora la Israel lilivyoruka juu ya kiwanda hicho kabla ya kiwanda kuripuka na kuwaka moto. Watu wawili waliuawa.

Sudan yaifikisha Israel mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Mjumbe wa Sudan kwenye Umoja wa Mataifa Daffa Alla Elhag amelitaka Baraza la Usalama liilaani Israel kwa shambulio hilo.

Kiwanda cha silaha cha Yarmouk kikiwaka moto baada ya mashambulizi.
Kiwanda cha silaha cha Yarmouk kikiwaka moto baada ya mashambulizi.Picha: Reuters

Mjumbe huyo amesema nchi yake inapinga vitendo hivyo vya kivamizi na inatumai Baraza la Usalama litailaani Israel kwani, shambulio hilo ni ukiukaji dhahiri wa amani, usalama na katiba ya Umoja wa Mataifa.

Mjumbe wa Sudan kwenye Umoja wa Mataifa pia ameilaumu Israel kwa kuwapa waasi wa Sudan silaha na pia kwa kusaidia kuwasafirisha viongozi wa waasi katika jimbo la Darfur.

Juu ya madai ya serikali ya Sudan msemaji wa jeshi la Israel ameeleza kuwa nchi yake haijibu madai kama hayo.Na msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Israel Yigal Palmor ameeleza kuwa Israel haina habari zozote juu ya mkasa huo.Lakini pia amesema kuwa Israel inayo haki ya kufanya mashambulio ya kijeshi ili kulinda maslahi yake.

Mnamo mwaka wa 2009 msafara wa malori ya Sudan yaliotuhumiwa kusafirisha silaha ulishambuliwa kaskazini mashariki mwa Sudan. Palikuwa na tuhuma kwamba silaha hizo zilikuwa zinapelekwa kwa wapiganaji wa Hamas katika ukanda wa Gaza.

Sudan pia iliilaumu Israel kwa shambulio hilo ambapo watu kadhaa waliuawa. Waziri wa habari na utamaduni wa Sudan ameliambia shirika la televisheni la Al jazeera kwamba nchi yake itawasilisha ushahidi kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuthibitisha kwamba Israel ilikishambulia kiwanda chake cha silaha mjini Khartoum.

Mwandishi: Abdu Mtullya/dpa/afpe/
Mhariri: Josephat Charo