1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mike Pompeo amewasili nchini Sudan,akitokea nchini Israel

Saleh Mwanamilongo
25 Agosti 2020

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani,Mike Pompeo yuko nchini Sudan,akitokea nchini Israel,kwa ziara ya kwanza ya kiongozi wa juu wa Marekani nchini humo.

https://p.dw.com/p/3hUy9
Abdel-Fattah Burhan, Mike Pompeo
Picha: picture-alliance/AP Photo/Sudanese Cabinet

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo amewasili leo nchini Sudan, akitokea nchini Israel, kwa ziara ya kwanza ya kiongozi wa juu wa Marekani nchini humo tangu kupinduliwa Omar al-Bashir mwaka jana. Ziara hiyo inalenga kurejesha mahusiano kati ya Sudan na Israel. 

Lengo kuu la ziara hiyo ya Mike Pompeo ni kujadili kurejeshwa kwa mahusiano kati ya Sudan na Israel, kufuatia makubaliano kama hayo na Umoja wa Falme za Kiarabu. Ndege aliyopanda Pompeo kutoka Tel Aviv hadi Khartoum ilikuwa ya safari ya kwanza ya moja kwa moja baina ya mataifa hayo. Sudan na Israel hazijawahi kuwa na uhusiano wa kidiplomasia.

Pompeo anakukutana mjini Khartoum na Waziri Mkuu Abdalla Hamdok. Kwenye ukarasa wake wa Twitter mara tuu baada ya mazungumzo yao, waziri mkuu Hamdok amesema kwamba walikuwa na mazungumzo ya moja kwa moja na ya wazi pamoja na waziri wa mambo ya nje wa Marekani.

Sudan kuondolewa vikwazo ?

Hamdok amesema kwamba wamejadili kuondolewa kwa Sudan kwenye orodha ya nchi zinazofadhili ugaidi, uhusiano baina ya Sudan na Marekani na Uungwaji mkono wa Marekani kwa serikali ya mpito ya kiraia. Sudan inatarajia kuondolewa kwenye orodha ya nchi iliyowekewa vikwazo na Marekani. Nchi hiyo inayotegemea usafirishaji wa mafuta, iliwekewa vikwazo vya kiuchumi toka miaka ya tisini.

Faisal Saleh, msemaji wa serikali ya Sudan amesema kwamba kwenye mazungumzo yao waziri mkuu wa Sudan amemuambia Pompeo kwamba serikali ya mpito haina mamlaka ya kuanzisha uhusiano rasmi na Israel.

Mike Pompeo waziri wa mamabo ya nje wa Marekani akiwa zaiarani nchini Isreal
Mike Pompeo waziri wa mamabo ya nje wa Marekani akiwa zaiarani nchini IsrealPicha: picture-alliance/AP Photo/D. Hill

Mnamo mwezi Februari, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu alikutana na Jenerali Burhan kwa siri nchini Uganda, ambapo baadaye wawili hao walitangaza kuanza hatua za kurejesha mahusiano kati ya nchi zao.

Chini ya utawala Omar El Bashir, aliyepinduliwa mwaka jana baada ya kuiongoza Sudan kwa miongo mitatu, nchi hiyo ilikuwa na uhusiano wa miaka mingi na kundi la ugaidi la Al-Qaida, lililokuwa likiongozwa na Osama Bin Laden. Osama aliishi na kupewa hifadhi ya miaka mingi nchini humo.

Diplomasia ya utawala wa Trump

Pompeo anatarajiwa pia kukutana na mkuu wa baraza la utawala, nchini Sudan, Jenerali Abdel-Fattah Burhan. Ziara hiyo ya Pompeo ilioanzia nchini Israel itampeleka pia Bahrain na kwenye Umoja wa Falme za Kiarabu.

Mwanzoni mwa mwezi huu, Israel na Umoja wa Falme za Kiarafabu zilifikia makubaliano ya kurejesha mahusiano chini ya upatanishi wa Marekani.

Utawala wa Trump unayachukulia makubaliano kati ya Umoja wa Falme za Kiarabu na Israel kuwa ni alama kubwa ya kihistoria kwenye siasa zake za nje, katika wakati huu Trump akiwania kuchaguliwa tena katika uchaguzi wa Novemba mwaka huu.