1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan yatishia kujibu uvamizi wa jeshi la Chad katika eneo la Dafur.

10 Aprili 2007

Serikali ya Sudan imesema watajibu kile walichodai ni uvamizi wa jeshi la Chad uliosababisha vifo vya wanajeshi 17 wa Sudan. Kadhalika Serikali ya Chad, ilikana madai hayo Malumbano haya yametokana na mahusiano yanayozorota baina ya nchi hizi jirani za Afrika ya kati.

https://p.dw.com/p/CHGa

Chad Imekana madai hayo ya kushambulia jeshi la Sudan,na badala yake kusema kuwa ilipambana tuu na wanamgambo wa Chad waliowashambulia kutoka upande wa Sudan.

Msejamji mmoja wa kijeshi wa Sudan naye alisema wanajeshi wa Chad waliokuwa na vifaru vinane na magari ya kijeshi mia moja waliingia kilomita mbili ndani ya mpaka wa Sudan,ishara kuwa walidhamiria kuyalenga majeshi yao.

Hatahivyo, waziri wa habari wa Chad Hourmadji Moussa Doumgor, alisemawaliwashambulia wanamgambo hao zaidi ya mia mbili waliokuwa katika eneo la Amdjerima. Waziri huyo wa serikali ya Chad alisema ni wanamgambo waliouwawa pamoja na wanajeshi wanane wa Chad pekee.

Kundi la maafisa wa Umoja wa Mataifa walioko Chad Mashariki walisema walipata maiti zimetapakaa katika vijiji vya Tiero na Marena, ambapo nyumba zilichomwa na wamagambo wa kiarabu. Umoja wa Mataifa umesema watu mia nne wamefariki katika mwezi uliopita kwenye mpaka huo wa Chad na Dafur.

Kadhalika rais wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki anatarajiwa kujadiliana na rais Omar al Bashir suala la Dafur katika ziara yake nchini humo. Nayo China iliyoonekana kuutetea utawala wa rais al Bashir, licha ya ripoti za ukiukaji wa haki za binadamu, sasa inabadili nia yake. Haya yanatokana na mazungumzo baina ya naibu waziri wa mambo ya nje wa China Dai Bingguo na naibu waziri wa mambo ya nje wa marekani John Negroponte kwa njia ya simu yaliolenga kuleta amani Dafur. Viongozi hao walijadili mapendekezo ya mpango wa amani wa Umoja wa Mataifa kupeleka majeshi ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa Dafur.

China ina ushawishi mkubwa juu ya Sudan kutokana na uhusiano wake wa kibiashara, na imekuwa ikikashifiwa kwa kuitetea Sudan baadili ya kuishinikiza kuyakubali mapendekezo ya amani.

Ni miezi miwili tuu imepita tangu rais wa Chad, Idriss Deby, na rais wa Sudan, Omar al-Bashir, walipoweka saini makubaliano ya amani nchini Libya. Waziri wamambo ya nje wa Sudan Ali al-Sadiq, alisema wamejaribu kudumisha amani lakini jeshi lao litasimama wima kupinga shambulizi lolote kutoka Chad.

Mahusiano mabaya baina ya Chad na Sudan yametokana na mauajai ya halaiki katika eneo la Dafur, ambapo zaidi ya watu laki mbili wamefariki katika miaka minne iliyopita. Vita hivyo vimesababisha pia zaidi ya Wachad laki moja kutoroka eneo hilo la mpakani na kupata hifadhi katika kambi za wakimbizi nchini Sudan.

Sudan imeilaumu serikali ya Chad kwa kufadhili makundi ya wanamgambo wa Dafur,huku Chad ikiilaumu serikali ya Sudan kwa kusababisha vurugu katika jamii zao za kiarabu.

Umoja wa mataifa umeidhinisha ufadhili wa wanajeshi elfu kumi na moja watakaopelekwa kurudisha amani kwenye mpaka huo.

Na licha ya wanajeshi elfu saba wa Umoja wa Afrika kuwepo kwenye eneo hilo la Dafur,ni dhahiri kuwa inahitajika mikakati zaidi kukabiliana na vita hivyo katika mpaka wa Chad Mashariki na Dafur Sudan.

Isabella Mwagodi