1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Suu Kyi aizuru Rakhine kwa mara ya kwanza

Grace Kabogo
2 Novemba 2017

Kiongozi wa Myanmar, Aung San Suu Kyi amezuru maeneo yaliyokumbwa na ghasia, ambako zaidi ya Waislamu laki tano wa Rohingya wamelazimika kuyakimbia makaazi yao kutokana na ukandamizaji wa kikatili unaofanywa na jeshi.

https://p.dw.com/p/2mssd
Myanmar Aung San Suu Kyi Besuch in Rakhine
Picha: Reuters

Suu Kyi aliwasili kwa kutumia helikopta ya kijeshi katika mji mkuu wa jimbo la Rakhine, Sittwe, huku usalama ukiwa umeimarishwa. Msemaji wa serikali ya Myanmar, Zaw Htay amesema Suu Kyi mbali na kutembelea mji wa mji wa Sittwe pamoja na eneo la kaskazini mwa Rakhine. Akizungumza baada ya kuwasili Sittwe kwa mara ya kwanza tangu kuzuka kwa mzozo huo, Suu Kyi aliwatolea wito kuepukana na ugomvi miongoni mwao.

Chris Lewa kutoka shirika linalofatilia miradi la Arakan, amesema kiongozi huyo wa Myanmar alikuwa akisimama njiani na kuzungumza na wakaazi wa maeneo hayo. Lewa amesema Suu Kyi amewataka wananchi hao kuishi kwa amani, na kwamba serikali iko kwa ajili ya kuwasaidia.

Serikali ya Myanmar imesema kuwa imeanza mchakato wa kuwarudisha mamia ya maelfu ya Waislamu wa Rohingya ambao wameikimbia nchi hiyo. Naibu Mkurugenzi wa serikali ya Rhakine, Tin Maung Swe amesema katika ziara hiyo ya siku moja, Suu Kyi ameongozana na watu 20 ambao wanasafiri katika helikopta mbili tofauti za kijeshi, wakiwemo maafisa wa serikali, jeshi na polisi.

Ukosoaji wa kimataifa

Suu Kyi, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, amekosolewa kimataifa kutokana na kushindwa kumaliza ghasia hizo na kulaani ukatili unaofanywa na jeshi la nchi hiyo, ambalo limeshutumiwa kwa kuhusika na vitendo vya ubakaji wa watu wengi, kuchoma moto mali za wananchi pamoja na kufanya mauaji tangu ghasia hizo zilipoanza mwishoni mwa mwezi Agosti.

Bangladesch | Rohingya-Flüchtlingslager rund um Cox's Bazar
Wakimbizi wa Rohingya wakiwa BangladeshPicha: DW/ P. Vishwanathan

Myanmar imekanusha madai kuhusu ''safisha safisha ya kikabila'', ikisema kuwa vikosi vyake vya usalama vimeanzisha operesheni ya kupambana na waasi, baada ya wanamgambo wa Rohingya kushambulia vituo 30 vya usalama kaskazini mwa Rakhine, Agosti 25.

Kiongozi huyo hakuwahi kuizuru Rakhine tangu alipochukua madaraka mwaka uliopita, baada ya kushinda katika uchaguzi wa mwaka 2015. Idadi kubwa ya wakaazi wa kaskazini mwa jimbo hilo ambalo linaujumuisha mji wa Maungdaw, walikuwa Waislamu hadi mzozo ulipozuka hivi karibuni.

Zaidi ya wananchi 600,000 wa Rohingya, ambao ni jamii ya watu wachache waliokuwa wanaishi katika miji mitatu kaskazini mwa Rakhine, wanaaminika kuwepo katika kambi za wakimbizi nchini Bagladesh. Shirika la kimataifa la kuwasaidia watoto, Save the Children, limesema kuwa moja kati ya watoto wanne wanakabiliwa na utapiamlo mkubwa.

Afisa wa usalama wa Bangladesh katika wilaya ya Cox Bazar, Meja Mohammed Iqbal amesema zaidi ya watu 4,000 wa Rohingya jana walivuka mto kuingia nchini humo. Hata hivyo, wakimbizi walioko katika kambi za Bangladesh wamesema jeshi la Myanmar limechoma moto vijiji vyao, ingawa Myanmar imewatupia lawama hizo wanamgambo wa Rohingya.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA, AP, Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga