1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria kwazidi kufukuta

Admin.WagnerD14 Mei 2012

Mapigano makali yametokea siku ya Jumatatu kati ya majeshi tiifu kwa rais Bashar Assad na waasi wa Free Syria katika mji wa al-Rastan ambapo wanajeshi 23 wa serikali wameripotiwa kuuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.

https://p.dw.com/p/14uy3
Mlipuko mjini Damascus
Mlipuko mjini DamascusPicha: AP

Kwa mujibu wa shirikia la uangalizi wa haki za binadamu la Syria, lenye makao yake mjini London, mapigano hayo yalianza mapema Jumatatu, baada ya vikosi vya serikali kuuvamia mji wa al-Rastan ulioko mkoani Homs, ambao ulitekwa na waasi tangu Januari mwaka huu.

Shirika la habari la Ujerumani, dpa, lilimnukuu mwanaharakati Omar Homsi akiyaelezea mashambulizi ya leo kuwa ni makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika mkoa wa Homs tangu kusainiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano mwezi April. Alisema waliskia makombora si chini ya 10 yakiangushwa kila dakika katika mji wa Homs na kwamba watu wawili waliuawa na sita wamejeruhiwa katika eneo la al- Rastan.

Taarifa zinasema majeshi ya serikali, yakisaidiwa na vifaru, pia yalivamia kijiji kimoja kinachokaliwa na Waislamu wa madhehebu ya Sunni magharibu mwa mji wa Hama na kuuwa raia saba usiku wa kuamkia leo.

Mapigano yatishia kuvuka mipaka
Mapigano mengine yameripotiwa katika mji wa Bandari wa Tripoli ,ulioko nchini Lubnan kati ya watu wa kabila la Alawite wanaomuunga mkono rais Assad na Waislamu wa madhehebu ya Sunni ambapo redio moja mjini humo imeripoti kuwa mtu mmoja aliuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa.

Siku ya Jumapili watu wanne waliuawa na wengine kumi walijeruhiwa katika machafuko kama hayo nchini Lubnan na kuzusha hofu ya kusambaa kwa mgogoro wa syria katika mataifa jirani.

Mwanajeshi wa Lubnan akiweka doria katika Mji wa Tripoli nchini humo.
Mwanajeshi wa Lubnan akiweka doria katika Mji wa Tripoli nchini humo.Picha: picture-alliance/dpa

Ubelgji yataka nguvu za jeshi zitumike
Wakati hayo yakijiri, Ubelgji imeitaka jamii ya kimataifa itafakkari njia mbadala ya kuwasilisha msaada kwa raia wa Syria, hata kama njia hiyo itahusisha matumizi ya jeshi.

Waziri wa mambo ya nje wa Ubelgiji, Didier Reynders, aliwaambia waandishi wa habari kabla ya kuanza kwa Mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya kuwa, licha ya umoja huo kuunga mkono mpango wa Amani wa Koffi Annan, mpango huo umeshindwa kufikia lengo lake la kusitisha mapigano.

Lakini Waziri wa Mambo ya Nje wa Luxenbourg Jean Asselborn, alitofautiana na mwenzake huyo pale aliposema kuwa nguvu za kijeshi si suluhisho la mgogoro wa Syria kwa sasa, na kwamba mpango wa Annan ndiyo njia mbadala pekee kwa sasa.

Sreet battles in Tripoli Lebanon Wanajeshi was Lubnan wakifanya doria katika kijiji cha Bab al-Tebbaneh mjini Tripoli nchini Lubnan.
Wanajeshi was Lubnan wakifanya doria katika kijiji cha Bab al-Tebbaneh mjini Tripoli nchini Lubnan.Picha: picture alliance/dpa

Ulaya yatangaza vikwazo vipya dhidi ya Assad
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya wanaokutana mjini Brussels nchini Ubelgiji, tayari wamekubaliana juu ya duru ya 15 ya vikwazo dhidi ya utawala wa rais Assad, wakipinga ukatili unaofanywa na utawala huo dhidi ya wapinzani.

Taarifa iliyotolewa wakati wa Mkutano wa mawaziri hao imesema wameweka vikwazo vipya dhidi ya utawala huo ingawa haikubainisha ni vikwazo vipi.

Lakini Mwanadiplomasia mmoja alithibitisha kuwa mawaziri hao waliidhinisha kuzuiwa mali na kuwekea vikwazo vya kusafiri dhidi ya kampuni mbili na watu watatu wanaoaminika kuwa wafadhili wakuu wa utawala wa Assad.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\AFPE\DPAE
Mhariri: Othman Miraji