1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria na Urusi zasitisha mashambulizi Aleppo

Sekione Kitojo
18 Oktoba 2016

Waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu amesema ndege za kivita za Urusi na Syria zimesitisha mashambulizi yake dhidi ya mji wa Aleppo kwa nia ya kuruhusu waasi na raia kuondoka kutoka mji huo.

https://p.dw.com/p/2RMuZ
Syrien Aleppo Bergung Opfer Luftangriff
Picha: picture-alliance/AA/I. Ebu Leys

Waziri  wa  ulinzi   wa  Urusi  amesema   kwamba  ndege za  kivita  za  Syria  na  Urusi  zimesitisha  mashambulizi yao  ya  anga  leo  katika  mji  uliozingirwa wa  Aleppo katika  matayarisho  ya  usitishaji  wa  muda  wa  mapigano ambao  Urusi  ilitangaza  kwamba  utaanza  baadaye  wiki hii.

Kwa  mujibu  wa  waziri  wa  ulinzi  wa  Urusi  Sergei Shoigu , usitishaji  wa  mashambulizi  ya  anga  utasaidia katika  kusafisha   njia  kwa  wanamgambo  kuondoka katika  maeneo  ya  mashariki  yanayodhibitiwa  na  waasi katika  mji  huo.

Mashambulizi  ya   anga  ya  majeshi  ya  Urusi  na  Syria dhidi  ya  Aleppo  yamesitishwa mapema  leo  asubuhi, Shoigu  alisema , akielezea  usitishaji  huo  wa  muda kuwa  ni  matayarisho  ya  kufungua  maeneo  maalum kwa   waasi  kuondoka  mjini  Aleppo  ifikapo  Alhamis, ambapo  Urusi  ilitangaza , usitishaji  mapigano  kwa sababu  za  kiutu  kati  ya  mbili  asubuhi  hadi  saa  kumi jioni  kwa  saa  za  Syria  kuruhusu  raia  na  wanamgambo kupata  njia  salama  ya  kupita  kutoka  katika  mji  huo.

Sergei Shoigu Verteidigungsminister Russland
Waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei ShoiguPicha: picture-alliance/dpa/R. Sitdikov

Mwakilishi  maalum  wa  Urusi  katika  Umoja  wa  mataifa Vitali Churkin  ambaye  anashikilia  kwa  sasa  urais  wa baraza  la  Usalama  la  Umoja  wa  Mataifa   wa kupokezana  alitangaza  hatua  hiyo  katika  Umoja  wa Mataifa jana.

"Sisi  tumetangaza  masaa  manane   ya  kusitisha mapigano. Nadhani  kwamba  usitishaji  mrefu  zaidi  kama masaa 48  ama  72 utahitaji aina  fulani  ya  makubaliano ya  pande zote."

Katika  wakati  huo , majeshi  ya  Syria  na  Urusi yatajizuwia  kuchukua  hatua  yoyote  ya  mashambulio. Waasi  wa  Syria , ikiwa  ni  pamoja  na  wanamgambo  wa al-Qaeda , pamoja  na  waliojeruhiwa  na  wagonjwa wataruhusiwa  kuondoka kwenda  katika  jimbo  jirani linalodhibitiwa  na  waasi  la  Idlib.

Syrien Gefechte um Dabiq
Wapiganaji wa kundi la Free Syrian Army wakipambana katika viunga vya mji wa Aleppo dhidi ya majeshi ya SyriaPicha: Getty Images/AFP/N. Al-Kathib

Ushawishi  wa  mataifa  kwa  waasi

Waziri Shoigu  ameongeza  kwamba , Urusi  inayaomba mataifa  yenye  ushawishi  kwa  waasi  mashariki  mwa Aleppo  kuwashawishi  viongozi  wao  kuacha  mapigano na  waondoke kutoka  mji  huo. Ameongeza  kwamba majeshi  ya  Syria  yatarejea  nyuma  hadi  katika   maeneo ambayo  yataruhusu  waasi  kupita  bila  matatizo  kwa wale  wenye  silaha kupitia  maeneo  mawili , ikiwa  ni pamoja  na  barabara  kuu  muhimu  ya  Castello.Juhudi hizo  za  Urusi  pia  zitatoa  nafasi  bora  kwa  mazungumzo baina  ya  wataalamu  wa  kijeshi  kutoka  mataifa  mbali mbali  ambayo  yanatarajiwa  kuanza  mjini  Geneva kesho Jumatano.

Msemaji  wa  katibu  mkuu  wa  Umoja  wa  mataifa Stephane Dujarric  alisema  baada  ya  kutopatikana  hatua ya  maana  katika  mashauriano  ya  faragha  yaliyofanyika katika  baraza  la  Usalama  la  Umoja  wa  Mataifa kuhusiana  na  suala  hilo  la  Syria kwamba  kilichotakiwa ni  kupata  uwezekano  wa  kupunguza matumizi  ya nguvu.

USA Treffen Syrien-Unterstützergruppe
Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergey Lavrov (kushoto) na John Kerry wa Marekani (kulia)Picha: picture-alliance/AP Photo/J. DeCrow

"Upunguzaji wa  ghasia , kupunguza  mapigano, usitishaji wa  aina  yoyote  ambao  utekelezaji  wake  utakuwa muhimu  sana. Tumekuwa  tukitoa  wito  wa  usitishaji  wa masaa  48 ili  kupeleka  misaada  ya  kiutu.

Katika  mkutano mwishoni  mwa  wiki  uliosimamiwa  kwa pamoja  na  waziri  wa  mambo  ya  kigeni  wa  Urusi Sergey Lavrov  na   John Kerry  wa  Marekani , mawaziri wa  mambo  ya  kigeni  wa  Saudi  Arabia, Uturuki  na Qatar  walisema  watafanyakazi  kuwatenganisha  makundi ya  upinzani  yenye  msimamo  wa  wastani  mjini  Aleppo kutoka  kundi washirika  wa  zamani  wa  al-Qaeda  katika mzozo  wa  Syria  kama  al-Nusra  Front.

Mwandishi: Sekione  Kitojo  / ape

Mhariri: Daniel Gakuba