1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria yagubika mkutano wa kilele wa G8

17 Juni 2013

Rais Barack Obama wa Marekani amewasili Belfast,Ireland ya kaskazini kuhudhuria mkutano wa kilele wa mataifa 8 tajiri kiviwanda na kuzungumza na kiongozi mwenzake wa Urusi Vladimir Putin kuhusu mzozo wa Syria.

https://p.dw.com/p/18r3C
Rais Obama Barack (kulia) na mkewe wakiwapungia mkono vijana katika ukumbi wa Wwater Front mjini BelfastPicha: Reuters

Mara baada ya kuwasili rais Barack Obama aliyefuata na mkewe Michelle na binti zake wote wawili,alipokelewa na waziri mkuu wa jimbo la Ireland ya kaskazini Peter Robinson na makamo waziri mkuu Martin McGuiness kabla ya kuwahutubia vijana zaidi ya 2000 kuhusu utaratibu wa amani katika jimbo hilo la Uingereza.

Baadae rais Obama atakwenda Lough Erne kuhudhuria mkutano wa kilele wa siku mbili wa kundi la mataifa tajiri zaidi kiviwanda G-8.Mzozo wa Syria unatarajiwa kugubika siku ya mwanzo ya mkutano huo,huku mazungumzo yakitarajiwa kuwa makali kati ya rais Barack Obama na kiongozi mwenzake wa Urusi,Vladimir Putin,mshirika wa jadi wa Damascus anaeonyesha hayuko tayari kuregeza msimamo wake kuelekea Syria.

Washington na Moscow wanaotaka kuitisha mkutano wa amani kuhusu Syria mwezi ujao mjini Geneva wamezidisha makali ya misimamo yao mnamo siku za hivi karibuni.Katika wakati ambapo nchi za magharibi zinapanga kuwapatia silaha waasi wa Syria kwa kile wanachosema "kuleta wezani sawa" wa nguvu kuelekea majadiliano,rais wa Urusi Vladimir Putin ameshaonya dhidi ya uwezekano kama huo."Nnafikiri tunakubaliana na fikra kwamba hakuna haja ya kuwaunga mkono watu ambao sio tu wanawauwa maadui zao,bali pia wanakula viungo vyao vya mwili hadharani na mbele ya kamera za televisheni." alisema rais Putin mwishoni mwa mazungumzo pamoja na waziri mkuu wa Uingereza David Cameron mjini London.Alikuwa akizungumzia kanda ya video iliyoonyeshwa mwezi uliopita inayoonyesha jinsi waasi wa Syria walivyokuwa wakila maiti ya mwanajeshi waliyemuuwa.

Uchumi wa dunia utamulikwa

G8 Gipfel in Lough Erne Golfhotel Irland
Eneo la Lough Erne unakofanyika mkutano wa kilele wa G8Picha: Reuters

Majadailiano kuhusu Syria yanafanyika katika wakati ambapo Iran,mshirika mwengine wa serikali ya rais Bashar al Assad imejipatia rais mpya ambae jumuia ya kimataifa inataraji atakuwa msuluhifu hasa katika suala la Syria na katika ugonvi kuhusu mradi wa kinuklea.

"Tutaitumia fursa ya kukutana viongozi wote wa G-8 kujaribu kufikia msimamo wa pamoja" amesema mwenyeji wa mkutano wa kilele wa G-8,waziri mkuu wa Uingereza David Cameron.

Kabla ya kuanza rasmi mkutano huo,viongozi wa Umoja wa Ulaya na Marekani watakutana na kutia saini mkataba wa biashara huru kati ya Umoja wa ulaya na Marekani.

Baadae viongozi watazungumzia jumla ya kiuchumi namna ilivyo.

Maandamano dhidi ya mkutano wa G8

G8 Gipfel in Enniskillen, Nordirland
Msichana anawapungia mkono askari wa usalama huko Enniskillen,Picha: Reuters

Takriban askari polisi elfu nane wanapiga doria kudhamini usalama wakati wa mkutano huo unaofanyika katika ngome ya zamani ya jeshi la IRA.Maandamano ya wapinzani wa G-8 yanatarajiwa kufanyika huko Enniskillen,mji ulioko karibu zaidi na jengo la mkutano la Lough Erne.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman