Syria yazusha malumbano Umoja wa Mataifa

Naibu katibu mkuu wa UN wa kitengo cha misaada ya kibinadamu ameilaumu Urusi na Syria kwa kutumia mabomu mjini Aleppo kuwashinikiza watu kujisalimisha na kuzua majibizano na Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa.

Majibizano hayo yalizuka baada ya naibu katibu mkuu wa Umoja wa mataifa anayeshughulikia misaada ya kibinadamu Stephen O´brien kulihutubia baraza la usalama la umoja wa mataifa kuhusu kile alichokitaja kuwa hali ya kuogofya katika eneo linalodhibitiwa na waasi la Mashariki mwa Aleppo ambapo watu 400 wameuawa na takriban watu elfu 2 kujeruhiwa katika muda wa chini ya mwezi mmoja wengi wao wakiwa watoto.

O'Brien aliilaumu Syria kwa kuuzingira mji huo na wakati huo huo kufanya kampeini ya mashambulizi ya mabomu pamoja na washirika wake wa Urusi katika kampeini ya maksudi ya kufanya maisha ya wakazi wa eneo hilo kuwa magumu zaidi.

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa ambaye pia ni rais wa sasa wa Baraza la Usalama la Umoja huo Vitaly Churkin alijibu akisema tuhuma hizo ni za kushangaza.

Mada Zinazohusiana

Churkin ameongeza kuwa inashangaza kwamba O’Brien alizungumzia kuhusu mabomu hayo kama yanayorushwa hivi sasa katika eneo la Mashariki mwa Aleppo wakati mashambulizi hayo yalisitishwa kwa siku saba sasa na pia kuleta dhana kwamba silaha za kemikali zimekuwa zikutumiwa katika mji huo .

Balozi wa Urusi katika UN na rais wa baraza la usalama kwa sasa Vitaly Churkin.

Alitaka kutolewe ushahidi na kumkashifu O’Brien kwa kushindwa kutaja kuwa ngome ya serikali ya eneo la Magharibi mwa Aleppo limekuwa chini ya kundi la wanamgambo la al- nusra lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaida.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa mataifa Samantha Power aliongezea sauti yake katika kuishutumu Urusi na kusisitiza kuwa ilihusika katika mashambulizi hayo kwa kutumia silaha ambazo hazijawahi kutumiwa hata katika uongozi wa kiimla nchini Syria. .

Stephen O’Brien alitoa wito kwa pande zote husika zinazotatiza usaidizi kufika katika eneo la Mashariki mwa Aleppo na mbinu mbali mbali za mateso kusitisha hatua hizo na kuruhusu maelfu ya watu waliokwama katika maeneo mengine 17 nchini humo kupata usaidizi. Marekani, Uingereza na Ufaransa zilimuunga mkono afisa huyo.

Mwandishi: Tatu Karema

Mhariri: Daniel Gakuba

Makala zaidi

Matukio ya Kisiasa | saa (0) nyuma

Hatua ya mwisho ya uchaguzi wa Bunge la Ulaya

Matukio ya Kisiasa | 24.05.2019

Ulaya yazungumzia kujiuzulu kwa May

Tufuatilie