1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taarifa ya michezo

Mohammed AbdulRahman3 Novemba 2006

Waziri wa michezo wa Kenya alivunja Shirikisho la kandanda nchini humo KFF.

https://p.dw.com/p/CHd0

Serikali ya Kenya imekivunja chama cha soka nchini humo KFF katika jitihada ya kumaliza vurugu ilioukumba mchezo wa kandanda nchini Kenya.

Waziri wa michezo Maina Kamanda alisema serikali imeunga kamati ya watu wanane itakayosimamia kwa muda mchezo huo katika hatua ya kumaliza kabisa mgogoro huo.

Shirikisho la soka la kimataifa FIFA liliisimamisha Kenya kushiriki katika mechi zote za kimataifa zinazoandaliwa na Shirikisho hilo tarehe 24 mwezi uliopita, baada ya kushindwa kuheshimu makubaliano yaliosainiwa na kutokana na kuzuka migogoro mipya ndani ya chama cha soka nchini humo.

Waziri Kamanda aliwaambia waandishi habari jana katika mkutano aliouitisha kufafanua hali ya mambo kwamba katika kipindi cha miaka mitatu iliopuita serikali ilitoa sio chini ya dola 834,500 moja kwa moja katika kandanda bila ya kuona mafanikio yoyote .

Alisema ameachwa kwenye mataa bila ya jengine la kueleza isipokua tu kwamba kandanda la Kenya linahitaji mwanzo mpya na hasa katika masuala ya usimamizi Kutokana na hayo akatangaza kuvunjwa kwa chama hicho cha soka na matawi yake yote nchini tena mara moja.

Kenya imekumbwa na mzozo wa kuwa na vyama viwili vya soka chama cha ligi ya kuu Premier League KPL na Shirikisho la kandanda KFF. KPL imetakiwa na FIFA kusimamia ligi ya timu 18 wakati KFF ilianzisha kampuni ya kusimamia ligi ya timu 20. Hivi sasa ligi zote mbili hazijulikani hatima yao.

Na Katika kandanda la kimataifa, Ronaldo, mbrazil anayelisakata dimba huko Uhispania na kilabu ya Real Madrid, amesema haelewi anapaswa kufanya nini ili aweze kurudi katika kikosi cha kwanza cha Kocha Fabio Capello.

Akizungumza na gazeti moja la kila siku la Uhispania ABC jana, Ronaldo mwenye umri wa miaka 30 na ambaye msimu uliopita aliipuka kidedea kwa kuwa mfungaji magoli mengi akiuona wavu mara 14 katika ligi ya Uhispania amekua akisumbuliwa na majeraha kadhaa.

Lakini hivi sasa wakati ambapo Capello amechukua hatamu za kuwa kocha , Ronaldo amepoteza nafasi yake kwa Mdachi Ruud van Nistelrooy aliyejiunga na real kutoka Manchester united ya England. Ronaldo alifanyiwa upasuaji mdogo wa goti baada ya fainali za kombe la dunia, na tangu wakati huo amecheza muda wa jumla wa dakika 100 katika ligi na mashindano ya kilabu bingwa ya ulaya Champions League. Binafsi ametamka “ Nafikiri Capello hana imani nami, kwani kama si hivyo ningecheza mechi nyingi zaidi”.