1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CDC yasema Afrika yaihitaji kujiimarisha dhidi ya corona

9 Julai 2020

Taasisi ya kuzuia na kudhibiti magonjwa ya Afrika CDC imesema kuwa bara la Afrika linapaswa kuongeza upimaji wa virusi vya corona na kuwafanya watu watumie zaidi barakoa wakati maambukizi yakipindukia nusu milioni.

https://p.dw.com/p/3f3nU
John N. Nkengasong Afrika Africa Centres for Disease Control
Picha: Getty Images/M. Tewelde

Katika muda wa wiki moja iliyopita, visa vipya vya maambukizi ya virusi vya corona barani Afrika viliongezeka kwa asilimia 24 huku takwimu kutoka kwa mataifa na shirika la afya duniani WHO zikionyesha kuwa bara hilo lina visa 512,499 vilivyothibitishwa vya ugonjwa wa COVID-19 na vifo 11930.

Wakati wa mkutano na wanahabari ulioandaliwa kwa njia ya video kutoka mjini Addis Ababa, mkuu wa taasisi ya kuzuia na kudhibiti magonjwa ya Afrika CDC John Nkengasong, amesema kuwa janga hilo la virusi linashika kasi na kwamba mataifa ya Afrika ambayo mengi hayana takwimu za kutegemewa, lazima yazingatie mbinu thabiti za kuhimiza uvaaji wa barakoa na kuimarishwa kwa hatua za uchunguzi na kufuatilia walioambukizwa.

Nkengasong ameongeza kwamba hatua hiyo itaokoa maisha. Ameyataja mataifa ya Misri, Nigeria, Afrika Kusini, Ghana na Algeria, kuwa yanayochangia asilimia 71 ya maambukizi.

Shirika la habari la CCTV latoa picha za maabara inayotajwa kuwa chimbuko la virusi vya corona

Wakati huo huo televisheni ya serikali nchini China imetangaza picha za video zinazoonyesha muonekano wa maabara ya taasisi ya kijeshi iliyoko mjini Wuhan, ambayo inatajwa kuwa chimbuko la virusi vya sasa vya corona.

Picha kutoka maabara hiyo ya P4 inayohusika na utafiti wa virusi, zinaaminika kuwa za kwanza kabisaa kuwahi kutolewa tangu ilipofunguliwa mwaka 2014. Lakini Televisheni hiyo haikutoa taarifa zaidi kuhusu shughuli za maabara hiyo.Mara kwa mara rais wa Marekani Donald Trump na maafisa wengine wakuu wa Marekani, wamekuwa wakirejelea madai kuwa virus vya corona huenda vilivuja kutoka maabara hiyo au hata vilitengenezwa kwa maksudi na taasisi hiyo.

Video hiyo ilijumuisha picha kadhaa za maeneo ya maabara hiyo huku ripoti hiyo ikisema kuwa kanuni za usalama zilizuia kusongea karibu zaidi na maabara hiyo, huku ikijikita zaidi katika kukemea tuhuma za uvujaji.

Wakati hayo yakijiri, shirika la afya duniani WHO ambalo limeshtumiwa vikali na Marekani kwa namna lilivyoshughulikia janga la virusi vya corona, leo limeunda jopo huru la kutathmini upya hatua lilizochukuwa kukabiliana na janga hilo.Jopo hilo huru la kushughulikia na kujitayarisha kwa majanga litaongozwa na aliyekuwa waziri mkuu wa New Zealand Helen Clark na aliyekuwa rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf. Akizungumza kutokea makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva, mkurugenzi mkuu wa shirika la WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus, alisema kuwa kupitia jopo hilo, ulimwengu utaweza kufahamu kile kilichotokea na pia suluhisho la kujenga maisha ya baadaye kwa pamoja.