1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tafauti baina ya Waarabu na Magharibi zaanza juu ya Libya

21 Machi 2011

Wakati mataifa ya Magharibi yakiishambulia Libya kutoka angani, inaonekana ya Jumuiya ya Mataifa ya Kiarabu juu tafsiri ya marufuku ya anga inagongana na ile ya hatua za kijeshi ya mataifa ya Magharibi.

https://p.dw.com/p/10dC8
Baadhi ya viongozi wa Arab League wakijadiliana juu ya Libya
Baadhi ya viongozi wa Arab League wakijadiliana juu ya LibyaPicha: picture-alliance/dpa

Tangu mwanzo ilikuwa wazi, kwamba hatua za kijeshi dhidi ya utawala wa Muammar Gaddafi ni jambo la hatari na kwamba matokeo yake hayafahamiki.

Ukweli huo ndio uliopo hadi sasa. Dikteta huyu wa Libya hajasalimu amri, badala yake anawashajiisha wafuasi wake kupigana vita dhidi ya malengo ya mataifa ya magharibi.

Vikosi vya Muungano wa Kimataifa yameanza hatua zake za kijeshi. Zinaushambulia utawala wa Gaddafi, lakini si kwa vikosi vya ardhini.

Vipi na lini vita vya anga na ardhini vitaletwa pamoja, bado haijulikani, lakini tusifanye kosa kudhani litakuwa jambo rahisi. Hivi vitakuwa vita vya muda mrefu na vitakavyogharimu maisha ya watu wengi.

Ndege ya kijeshi ya Ufaransa ikielekea kushambulia Libya
Ndege ya kijeshi ya Ufaransa ikielekea kushambulia LibyaPicha: dapd

Hata hivyo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikuwa limelichukulia jambo hili vyema, pale liliposema kwamba, haliwezi kukubaliana na vitendo vya dikteta kuwaua raia wake mwenyewe.

Lakini jumuiya ya kimataifa ilipaswa kuonesha kuwa, mshikamano wake na umma unaodai uhuru na haki katika ulimwengu wa Kiarabu si maneno matupu.

Kwa hivyo, jumuiya hii ilikuwa imekabiliwa na wakati mgumu sana kimaadili, ndio maana ilikuwa lazima kwake kufanya maamuzi makubwa na magumu pia.

Hatari inakuja pale Marekani, Ufaransa na Uingereza zinapolazimisha ushiriki na uwepo wa moja kwa moja mataifa ya Kiarabu katika operesheni hii.

Ni kweli kuwa ni Jumuiya ya Mataifa ya Kiarabu iliyokuwa kimbelembele kutaka Libya iwekewe marufuku ya anga, na ni kweli kuwa baadhi ya wanachama wa Jumuiya hiyo, kama vile Qatar na Imarat, zimejishirikisha moja kwa moja kijeshi kwenye operesheni hii.

Lakini hili nalo lisichukuliwe kijuujuu tu, maana uendeshaji wa operesheni nzima uko chini ya makamanda wa mataifa ya magharibi, na bado haijulikani ni lini mataifa ya Kiarabu yenyewe na peke yake yanaweza kukabidhiwa dhamana ya kuendesha operesheni hii.

Matokeo ya mashambulizi ya Marekani, nchini Libya
Matokeo ya mashambulizi ya Marekani, nchini LibyaPicha: dapd

Na hapa hasa dipo inapokuja hiyo shaka ya uhalali wa misheni hii ya kijeshi katika eneo hili. Ikilinganishwa na uvamizi wa majeshi ya ushirika nchini Iraq na Afghanistan, misheni hii dhidi ya Libya ilipata uungwaji mkubwa zaidi kutoka ulimwengu wa Kiarabu kuanzia mwanzoni. Watu wengi walionesha mshikamano wao na waasi dhidi ya utawala wa Gaddafi.

Lakini hali hii inaweza kubadilika haraka, baada ya picha za maafa ya kiraia yanayotokana na mashambulizi ya Marekani, kurushwa kwenye televisheni au mtandao wa YouTube.

Japokuwa bado haujaonesha mbadala wa hatua za kuchukuliwa, tayari Jumuiya ya Mataifa ya Kiarabu umeshaanza kupingana na mashambulizi ya majeshi ya Muungano wa Kimataifa, kwa madai kuwa hicho sicho kitu walichokubaliana.

Jambo hili linagonga kengele ya tahadhari, kwamba muda si mrefu kuanzia sasa, zile hasira ambazo Waarabu walizionesha dhidi ya tawala zao, zitageuka na kuelekezwa dhidi ya mataifa ya magharibi. Na kuanzia hapo wataziona tawala zao kuwa ziko sawa.

Mwandishi: Rainer Sollich/ZPR
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Othman Miraji