1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tahadhari ya vita yawekwa Ukraine

1 Mei 2014

Majeshi ya Ulinzi ya Ukraine yako katika tahadhari kamili ya vita dhidi ya uwezekano wa kuvamiwa na Urusi wakati serikali ikikiri haina uwezo kuwazuwiya waasi kuimarisha udhibiti wao mashariki mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/1Brww
Jeshi la Ulinzi la Ukraine.
Jeshi la Ulinzi la Ukraine.Picha: picture-alliance/AP Photo

Waasi wamevamia jengo la polisi la mkoa na ukumbi wa halmashauri ya jiji katika mji wa mashariki wa Ukraine wa Gorlivka na kufanya zaidi ya miji 12 tayari kuwa chini ya mikono ya waasi.

Unyakuzi huo mpya unafuatia mapambano karibu na mji wa Lugansk yaliotokea hapo Jumanne wakati mamia ya waandamanaji wanaoiunga mkono Urusi wakiongozwa na umati wa watu waliokuwa na silaha walipokishambulia kituo cha polisi.

Hapo jana waasi wameacha kulizingira jengo la makao makuu baada ya mkuu wa polisi kuahidi kuwa atajiuzulu, wakati vyombo vya habari vikirepoti kwamba wanamgambo wanaoiunga mkono Urusi wamelinyakuwa jengo la halmashauri ya jiji katika mji wa Alchevsk bila ya kukabiliwa na upinzani wowote ule.

Taifa lajiandaa kwa vita

Rais wa mpito wa Ukraine Oleksandr Turchynov ameliambia baraza lake la mawaziri kwamba taasisi za usalama za taifa zimekuwa hazina uwezo wa kuzuwiya waasi wasivamie majengo ya serikali katika eneo la machafuko mashariki ya nchi hiyo.

Rais wa mpito wa Ukraine Alexandr Turtschynov.
Rais wa mpito wa Ukraine Alexandr Turtschynov.Picha: Reuters

Amesema majeshi ya ulinzi ya taifa yamewekwa katika tahadhari kamili ya vita kukabiliana na kile alichokiita kuwa tishio la kweli la Urusi kuanzisha vita dhidi ya jimbo hilo la zamani la Muungano wa Kisovieti.

Wakati hali hiyo ya mvutano ikiongezeka serikali imesema imemkamata mwambata wa kijeshi wa Urusi kwa tuhuma za ujasusi na kumuamuru aondoke nchini humo.

Shirika la habari la Urusi Interfax tawi la Ukraine limeikariri wiraza ya mambo ya nje ya Ukraine ikisema mwambata huyo wa kijeshi wa kikosi cha majini wa ubalozi wa Shirikisho la Urusi ametangazwa kuwa mtu asiyetakiwa kuwepo nchini humo kutokana na vitendo vyake ambavyo haviendani na hadhi ya kidiplomasia.Imesema mwanadiplomasia huyo ambaye hakutajwa jina alikamatwa hapo jana wakati akishiriki kwenye vitendo vya kijasusi na itabidi aondoke nchini humo.

Merkel aitishia Urusi kwa vikwazo zaidi

Hapo jana Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ameitishia Urusi kwa vikwazo zaidi. Amesema iwapo yote hayo wanayoyafanya yatashindwa kuzaa matunda,hawapaswi kujiepusha na kukubali ukweli kwamba vikwazo zaidi vinahitajika.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.Picha: Reuters

Mataifa ya magharibi yamekuwa yakiishutumu Urusi kwa kuchochea mzozo huo wa Ukraine na kuwaunga mkono waasi na wameiwekea vikwazo nchi hiyo kujaribu kuifanya serikali ya nchi hiyo iachane na msimao wake huo.

Wakati viongozi wapya wa serikali ya Ukraine wakipigania kuzuwiya kunyakuliwa kunakoinyemelea kwa eneo la mashariki mwa nchi hiyo na waasi wenye asili ya Urusi, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limeidhinisha msaada wa dola bilioni 17 kwa nchi hiyo.

Ukraine inakabiliwa na matatizo makubwa ya kifedha na Rais Vladimir Putin wa Urusi ametishia usambazaji muhimu wa gesi kwa nchi hiyo iwapo haitolipa kwa haraka deni lake la dola bilioni 3.5.

Takwimu zilizitolewa hapo jana zinaonyesha kwamba mzozo huo umethiri uchumi wa nchi hiyo ambao tayari ni dhaifu kwamba pato la ndani ya nchi limeshuka kwa asilimia mbili katika miezi mitatu ya kwanza ya mwaka huu kulinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2013.

Mwandishi : Mohamed Dahman /AFP/Reuters/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman