1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Takribani mateka wote wa ndege ya Misri waachiwa huru

Mohammed Khelef29 Machi 2016

Ndege ya shirika la ndege la Misri bado inaendelea kushikiliwa na mtekaji nyara aliyeilazimisha kutua nchini Cyprus katika tukio la aina yake ambalo maafisa wanasema halina uhusiano na ugaidi.

https://p.dw.com/p/1ILF4
Ndege ya shirika la ndege la Misri, EgyptAir, ikiwa imetekwa na kulazimishwa kutua nchini Cyprus.
Ndege ya shirika la ndege la Misri, EgyptAir, ikiwa imetekwa na kulazimishwa kutua nchini Cyprus.Picha: Reuters/Y. Kourtoglou

Taarifa za hivi karibuni kabisa zinasema kati ya watu 81 waliokuwamo kwenye ndege hiyo, ni saba tu waliobakia, huku wengine wote wakiwa wameshaachiwa huru. Miongoni mwa waliobakia ni rubani, msaidizi wake, abiria wanne na mtekaji nyara mwenyewe.

Waziri wa Usafiri wa Anga wa Misri, Sharif Fathy, amewaambia waandishi wa habari muda mfupi uliopita kuwa bado hawajaweza kuthibitisha madai ya mtekaji nyara kuwa amejifunga mkanda wa mabomu, ingawa kwa sababu za kiusalama wanachukulia kuwa ni kweli.

Muda mfupi uliopita, picha za moja kwa moja za televisheni kutoka uwanja huo, zimewaonesha watu wengine watano wameonekana kutoka kwenye ndege hiyo.

Shirika la habari la Cyprus limewanukuu maafisa wa usalama wakisema lengo la mtekaji nyara ni la kibinafsi na wala si ugaidi kama ilivyokuwa imehofiwa hapo awali.

Mamlaka nchini Misri zimekataa kutaja majina na uraia waliobakia kwenye ndege hiyo pamoja na mtekaji nyara mwenyewe.

Misri yapinga jina la mtekaji nyara

Fathy alipinga vikali taarifa zilizosambaa kwenye vyombo vya habari kuwa mtekaji nyara huyo ni Profesa Ibrahim Abdel Tawwab Samaha wa Chuo Kikuu cha Alexandria nchini Misri, ambaye ameomba kukutanishwa na mkewe wa zamani anayeishi katika kijiji kilicho karibu na uwanja wa ndege huo.

Ndege ya shirika la ndege la Misri, EgyptAir, ikiwa imetekwa na kulazimishwa kutua nchini Cyprus.
Ndege ya shirika la ndege la Misri, EgyptAir, ikiwa imetekwa na kulazimishwa kutua nchini Cyprus.Picha: Reuters/Y. Kourtoglou

Rais Nicos Anastasiades wa Cyprus amesema sababu hasa ya utekaji nyara huo haijafahamika, lakini alithibisha kuwa haina uhusiano wowote na ugaidi, huku afisa mmoja wa serikali yake, ambaye hakutaka kutajwa jina, akisema inaonekana mtekaji nyara anataabishwa na suala la kimapenzi.

Ndege hiyo iliyokuwa ikielekea Alexandria kuelekea Cairo ilikuwa na abiria 21 wa kigeni wakiwemo Wamarekani wanane, Waholanzi wanne, Waingereza wanne na Mfaransa mmoja.

Tukio hili linazidi kuzusha mashaka juu ya usalama kwenye viwanja vya ndege nchini Misri, ikiwa ni miezi mitano tangu ndege ya Urusi kuanguka kwenye eneo la Sinai dakika chache baada ya kuruka kutoka uwanja wa ndege wa Sharm el-Sheikh.

Watu wote 224 waliokuwamo waliuawa kwa kile ambacho Urusi inasema ni bomu lililoingizwa kwenye ndege hiyo, ambalo kundi la kigaidi la Dola la Kiislamu lilidai kuhusika.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga