1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taliban na Pakistan kujadili mazungumzo yaliyositishwa

Lilian Mtono
2 Oktoba 2019

Kundi la wanamgambo la Taliban limetuma ujumbe wa juu katika mji mkuu wa Pakistan, ikiwa ni sehemu  ya ziara za kikundi hicho katika mataifa ya Urusi, Iran na China.

https://p.dw.com/p/3QbxU
Russland Moskau Afghanistan-Gespräche Mullah Baradar Taliban
Picha: picture-alliance/dpa/TASS/S. Fadeichev

Msemaji wa Taliban Suhail Shaheen aliandika kwenye ukurasa wa twitter kwamba ujumbe huo unaoongozwa na Mullah Abdul Ghani Baradar, mmoja wa waasisi wa kundi hilo la waasi utajadiliana masuala muhimu na maafisa wa Pakistan katika mji mkuu Islamabad.

Pakistan imekuwa ikiwaunga mkono Taliban tangu kuasisiwa kwa kundi hilo katikati ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Afghanistan mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Afisa mmoja wa Taliban ambaye hakutaja jina lake amesema ujumbe huo wa Taliban huenda ukazungumza na uongozi wa Pakistan kuhusu sababu za kuvunjika kwa mazungumzo na Marekani yaliyolenga kupatikana kwa makubaliano ili hatimaye Marekani na mataifa mengine ya nje yaondoe wanajeshi wao nchini humo. 

Ujumbe huo pia unapanga kufuatilia matamshi ya hivi karibuni ya waziri mkuu wa Pakistan Imran Khan kabla ya mkutano kati yake na rais Donald Trump wa Marekani mjini New York, kwamba atajaribu kumshawishi rais huyo kurejea kwenye mazungumzo. Hata hivyo haikuelezwa iwapo watakutana na waziri mkuu huyo.

Russland l Politischen Führer der Taliban treffen zu Gesprächen in Moskau ein
Ujumbe wa Taliban ukiwasili kwenye mazungumzo ya amani nchini Urusi.Picha: picture alliance/AP Photo/A. Zemlianichenko

Rais Donald Trump alisitisha mazungumzo mwezi uliopita.

Ziara hiyo pia inakuja baada ya vyombo vya habari vya Pakistan kuripoti kwamba mjumbe maalumu ya rais Donald Trump kwenye mazungumzo ya amani ya Afghanistan Zalmay Khalilzad yuko Islamabad kwa mazungumzo na maafisa wa Pakistan. Hata hivyo si wizara ya mambo ya kigeni ama ubalozi wa Marekani waliothibitisha kuhusu zara hizi.

Marekani pamoja na serikali ya Afghanistan inayoiunga mkono kwa muda mrefu wamekuwa na wasiwasi kwamba Pakistan imeendelea kulisaidia kundi hilo, ili kuzuia kusambaa kwa ushawishi wa India nchini Afghanistan, licha ya kwamba Pakistan inakana madai hayo.

Matangazo ya Mchana 28.09.2019

Mwezi uliopita, Marekani na Taliban walisema walikaribia kufikia makubaliano, licha ya wasiwasi miongoni mwa maafisa wa usalama wa Marekani pamoja na waliopo ndani ya serikali ya Afghanistan kwamba kuondolewa kwa wanajeshi wa Marekani kunaweza kuitumbukiza nchi hiyo kwenye mzozo mkubwa zaidi na kufungulia njia uasi wa makundi ya wanamgambo.

Rais Trump alisitisha mazungumzo hayo na Taliban mwezi uliopita yenye lengo la kumaliza vita hivyo vilivyodumu kwa miaka 18, kufuatia kifo cha mwanajeshi wa Marekani na watu 11 katika shambulizi la bomu mjini Kabul.

Wakati huohuo, wanamgambo hao wa Taliban wameendelea kufanya mashambulizi, hata baada ya taifa hilo kufanya uchaguzi wa urais Jumamosi iliyopita. Hata hivyo, Pakistan imesema itaendelea kuwashawishi Taliban kufanya mazungumzo na Kabul, baada ya kufikia makubaliano ya aina yoyote na Washington.