1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania: Kesi ya Eric Kabendera yatajwa

1 Agosti 2019

Mawakili wa mwandishi habari za uchunguzi wa Tanzania Erick Kabendera wamepeleka  shauri katika mahakamani ya Kisutu mjini Dar es Salaam kutaka mteja wao afikishwe mahakamani 

https://p.dw.com/p/3N8QP
Tansania DW-Interview mit Shilinde Swedy, Rechtsanwalt von Edward Kabendera
Picha: DW/H. Bihoga

Hii ni baada ya Kabendera kushikiliwa na vyombo vya usalama takriban siku tatu zilizopita bila ya kupewa dhamana. Kabendera hakuwasili mahakamani kama wengi walivyotaraji kumuona isipokuwa mawakili wake walimuwakilisha, ambapo mwendo wa saa tatu asubuhi lilianza kusikilizwa shauri  hilo na kudumu kwa takriban dakika ishirini huku hoja kubwa wakiisaka haki ya dhamana kwa mteja wao.

Shauri hilo lililowasilishwa na wakili kutoka mtandao wa watetezi wa haki za binadamu baada ya mteja wao kushikiliwa na jeshi la polisi kwa takriban siku tatu kwa madai kuchunguza uraia wake baada ya uhamiaji kumtilia shaka juu ya uraia wake hivyo wanamshikilia kwa ajili ya mahojiano.

Katika maombi hayo namba 14 ya mwaka 2019 yaliyofunguliwa Julai 30, wakili wa Kabendera amesema kuwa saa 24 zimeshapita, hivyo anapaswa kufikishwa mahakamani dhidi ya tuhuma zozote zinazomkabili kwa ajili ya haki zake za msingi ikiwemo dhamana kwani kosa linadhaminika.

Upande wa serikali watakiwa kuwasilisha kiapo kinzani

Katika majibu ya Serikali, kupitia Wakili wa Serikali Wankyo Simon aliiomba mahakama iwape muda mpaka August 7, 2019 kwa ajili ya kuwasilisha kiapo kinzani katika maombi hayo, huku upande wa utetezi ukiomba Agosti 2, 2019.

Hata hivyo baada ya kusikilizwa kwa pande zote mbili hakimu Rwizile ameutaka Upande wa Serikali kuwasilisha kiapo kinzani Augusti 5, 2019 saa saba mchana, kujibu hoja kuhusu kukamatwa kwa Mwandishi huyo wa Habari za Uchunguzi, Erick Kabendera.

Nje ya mahakama wakili wa Erick Kabendera Shilinde Swedy ameiambia DW kuwa hadi sasa wanaheshimu maamuzi ya mahakama na watasuribi siku ya juma tatu kwa ajili ya kubishana hoja kisheria kwa lengo la kuhakikisha mteja wao anapata dhamana.

Kukamatwa kwa Kabendera kulizua hofu na wasawasi miongoni mwa wengi na hata kuanzishwa kwa harakati mbalimbali za kuhakikisha ana kuwa huru, wakati zile za mtandaoni zilionesha kuwa na nguvu zaidi hata jeshi la polisi kutoka hadharani na kusema linamshikilia kwa ajili ya mahojiano juu ya uraia wake.Swali la wengi linasalia je yu hali gani huko aliko, ukizingatia zilitajwa kutumika nguvu wakati wa kumkamata?

Erick Kabendera mwandishi wa hababri za uchunguzi alichukuliwa na jeshi la polisi nyumbani kwake mwanzoni mwa juma hili.

Mwandishi: Hawa Bihoga Dw Dar es salaam