1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania kumpokea Obama

1 Julai 2013

Rais wa Marekani Barack Obama leo anatazamiwa kuwasili nchini Tanzania kwa ziara ya siku mbili ikiwa ni kituo chake cha mwisho barani Afrika

https://p.dw.com/p/18z1I
Rais Obama akiwa Afrika Kusini na mkewe Michelle Obama
Rais Obama akiwa Afrika Kusini na mkewe Michelle ObamaPicha: Getty Images

Rais Obama akiwa ameandamana na Mkewe Michelle Obama na wanawe atawasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere nyakati za saa nane na dakika 20.

Kumekuwa na hamu kubwa kutoka kila kona kuhusiana na ziara ya kiongozi huyo ambaye msafara wake unaambatana na kundi la wafanyabiashara na pamoja na wanadiplomasia.

Atapowasili kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere, Rais Obama atapokelewa na mwenyeji wake Rais Jakaya Kikwete na kisha kukagua gwaride kabla ya mizinga 21 kufyetuliwa, kama ishara ya U-amri Jeshi Mkuu

Baadaye viongozi hao wawili watakuwa na majadiliano ya faragha ikulu kabla ya kukutana na waandishi wa habari kwa ajili ya kujadilia masuala mbalimbali.

Rais Jakaya Kikwete na rais wa zamani wa Marekani George Bush pia yuko Tanzania
Rais Jakaya Kikwete na rais wa zamani wa Marekani George Bush pia yuko TanzaniaPicha: AP

Kumekuwa na kundi kubwa la waandishi wa haabri, ambao baadhi yao wamewasili jana kutoka nchi za magharibi. Kundi jingine la waandishi wa habari kutoka nchini Marekani liliwasili leo mchana kwa ndege maalumu kwa ajili ya kufuatilia ziara hii.

Ujio wa rais Obama unakuja ikiwa imepita miezi michache tu tangu kuwasili nchini kwa Rais wa China XI Jinping ambaye alitumia Jukwaa la Tanzania kunadi sera zake za mambo ya nje. Rais wa China alifaulu kuishawishi Tanzania na kufanikisha kusainiwa kwa mikataba 17 ya ushirikiao ikiwemo ile inayohusu miundo mbinu, biashara.

Pamoja na kwamba ikulu ya Dar es salaam haijasema lolote kuhusiana na ziara hii, lakini wachunguzi wa mambo wanaona kuwa, Rais Obama huenda akatumia vyema karata yake ya ushawishi na kufanikiwa kupata mikataba minono hasa katika maeneo ya gesi na kilimo.

Wakati huu kunaposubiriwa kuwasili kwa kiongozi huyo wa Marekani, hali ya ulinzi imeimarishwa katika maeneo yote ya mkoa wa Dar-esalaam, na bara bara kadhaa zimefungwa kwa muda.

Mkuu wa Mkoa huo, Sadiq Mecky Sadiq amesema kuwa kufungwa kwa bara bara hizo kumelenga kurahisisha shughuli za ulinzi.

Rais wa China Xi Jinping hivi karibuni akiwa Tanzania
Rais wa China Xi Jinping hivi karibuni akiwa TanzaniaPicha: Reuters

Pamoja na hayo Jiji la Dar-esalaam, limepambwa na bendera za mataifa yote mawili, huku zikikolezwa na picha za Rais Obama zilizobandikwa kila kona. Ratiba ya Rais Obama inaonyesha kuwa baada ya kukutana na waandishi wa habari atakuwa na mkutano na jumuiya ya wafanyabiashara baadaye leo jioni na kesho atahitimisha ziara yake kwa kutembelea Ofisi za ubalozi wa Marekani na baaadaye kwenda kwenye kituo kimoja cha uzalishaji Umeme kabla ya kupanda ndege kurejea nyumbani Washington.

Kandoni mwa hayo, wake wa marais barani Afrika wanatazamiwa kuwa na kongamano maalumu ambalo limeandaliwa na wakfu wa rais wa zamani wa Marekani George W. Bush ambaye naye yupo nchini akiwa ameambatana na mkewe Laura Bush na mke wa aliyekuwa waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair.

Mwandishi:George Njogopa

Mhariri:Yusuf Saumu