1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania: Magufuli akutana na viongozi wa upinzani

George Njogopa3 Machi 2020

Rais wa Tanzania John Magufuli amekutana Jumanne na viongozi wa vyama vya upinzani katika kile kilichoelezwa kuwa ni majadiliano ya masuala ya kitaifa huku taifa hilo likijiandaa kuelekea katika uchaguzi mkuu.

https://p.dw.com/p/3YoEA
John Pombe Magufuli , Maalim Seif Shariff Hamad, Tansania
Picha: Tanzania Presidential office

Tanzania: Magufuli akutana na viongozi wa upinzani

Viongozi wa vyama hivyo vya upinzani wamekaribishwa ikulu kwa nyakati tofauti na picha za vidio zilizotolewa na Ikulu zinamwononesha mwanasiasa wa siku nyingi na mshauri mkuu wa chama cha ACT Wazalendo Maalim Seif akifurahia jambo na Rais Magufuli na wawili hao wakionekana kuwa katika hali ya bashasha kubwa.

Maalim Seif aliyewania urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama cha CUF zaidi ya mara tatu, akilalamika kupokwa ushindi wake ameutaja mkutano wake wa Jumanne na Rais Magufuli kuwa ni wa mafanikio makubwa.

"Namshukuru rais kwamba kakubali tukutane tuzungumze mambo ya maslahi ya nchi yetu. Namshukuru sana,"amesema Sharif.

President of Tanzania John Pombe Magufuli and Maalim Seif Shariff Hamad
Rais John Pombe Magufuli akiwa na Maalim Seif Sharif Hamad (Ikulu ya Rais Tanzania)Picha: Tanzania Presidential office

Mbali na Maalim Seif, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na wanasiasa wengine. Na kulingana na picha zilizotolewa na Ikulu, amekutana na Mwenyekiti wa chama cha wananchi Cuf, Profesa Ibarahim Lipumba na Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi James Mbatia.

Tanzania: Magufuli akutana na viongozi wa upinzani

Hakuna picha yoyote ya vidio iliyotolewa kuwaonyesha wanasiasa hao wawili wakizungumzia mkutano wao na Rais Magufuli, lakini alipokutana baadaye na waandishi wa habari katika ofisi za chama chake, mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi Mbatia alidokeza baadhi ya mambo aliyojajadili wakati akiwa Ikulu. Amesema suala kuhusu uchaguzi mkuu ujao ni miongoni mwa mambo ambayo yalijadiliwa kwenye mkutano huo.

"Leo nimeitwa na mheshimiwa rais nimemuuliza nchi hii tunaipeleka wapi? Akaniambia kama nilivyowaambia mabalozi, ninaendelea kusisitiza uchaguzi wa mara hii utakuwa ni wa huru na wa haki, " ameeleza Mbatia.

John Pombe Magufuli und Ibrahim Lipumba Tansania
John Pombe Magufuli akiwa na Ibrahim Lipumba Picha: Tanzania Presidential office

Hadi sasa bado haijafahamika kama viongozi wa vyama vingine vya siasa wameitwa Ikulu ikiwamo chama kikuu cha upinzani Chadema ambacho mara zote kimekuwa kikiimba wimbo wa kutaka tume huru kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba.

Mikutano hiyo ya Rais Magufuli huenda ikawa hatua muhimu ya kukaribisha maridhiano ya wanasiasa hasa wakati huu wa kuelekea katika uchaguzi Mkuu.

Suala la kutaka maridhiano ya kitaifa limewahi kuibuliwa na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe wakati chama chake kilipohudhuria na kushiriki kwa mara ya kwanza kilele cha sherehe za uhuru wa Tanganyika zilizofanyika Disemba 9 jijini Mwanza.