1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yafafanua kuhusu sakata la Ngorongoro

18 Februari 2022

Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari Tanzania wamembana Waziri wa Maliasili na Utalii Dokta Damas Ndumbaro wakimtaka afafanue kuhusu sakata la wakaazi wa Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro

https://p.dw.com/p/47F5i
Tansania Ngorongoro-Kraters Massai-Großfamilie
Picha: Imago/Plusphoto

Wakati sakata la Watanzania wanaoishi ndani ya hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro likiwa bado halijapata suluhisho, wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini wamembana Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania, Dokta Damas Ndumbaro wakimtaka afafanue kuhusu utata wa kauli za Waziri Mkuu nchini Tanzania Majaliwa Kassim Majaliwa kuhusu wakazi hao kuhama au kutokuhama katika eneo hilo. 

Katika kikao chao kilichofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Maliasili na Utalii jijini Dar es Salaam leo, wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini walikutana na kuzungumza na Waziri wa wizara hiyo Dokta Damas Ndumbaro ambapo pamoja na mambo mengine walimtaka afafanue kuhusu utata wa kauli ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyoitoa akiwa katika Kata ya Ngorongoro na Kata ya Loliondo, zilizopo wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha.

Kassim Majaliwa, Premierminister von Tansania
Kauli ya Majaliwa ilizusha utata kuhusu NgorongoroPicha: Büro des Premierministers von Tansania

Awali Waziri Mkuu akiwa Kata ya Ngorongoro, aliwaambia wananchi na wadau kuwa serikali haitawahamisha wakazi hao na wakati huo huo akiwa katika Kata ta Loliondo aliwataka wananchi wa eneo hilo wajiandikishe kuhama kwa hiari na kwamba serikali itagharamia mahitaji yao.

Mhariri wa Habari wa gazeti la Mwananchi, Lilian Timbuka alimuhojia Waziri Ndumbalo na kumtaka azungumzie utata wa kauli hizo za waziri mkuu. Akijibu hoja hiyo Waziri huyo mwenye dhamana ya Maliasili na Utalii nchini Tanzania, amesema hitimisho litafikiwa baada ya serikali kufanya majadiliano na mjadala mpana kati ya wananchi, wadau na serikali.

Wahariri wameitaka serikali itoe suluhisho la kudumu, kuhusu ongezeko la binadamu katika eneo la hifadhi hiyo ya Taifa yenye wakazi zaidi ya 73,000 jambo lililosababisha mgogoro wa muda mrefu na kuzusha wasiwasi kuwa huenda hifadhi ikatoweka.

Ngoro Tansania
Ngorongoro ni mojawapo ya mbuga maarufu AfrikaPicha: CC BY-SA 2.0/ Chin tin tin

Pamoja na sakata la Ngorongoro, wahariri pia walimhoji Waziri Ndumbaro kuhusu utoaji wa vibali vya uwindaji na ongezeko la ujangili ndani ya hifadhi. Mhariri na mjumbe wa kamati tendaji wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF) Neville Meena alisema.

Hifadhi ya Ngorongoro ilianzishwa mwaka 1959 na serikali ya kikoloni baada ya watu wa kabila la Maasai kuhamishwa kutoka hifadhi ya Serengeti. Hata hivyo, baada ya Ngorongoro kuwa hifadhi mseto ya wanyama na binadamu kwa muda mrefu, kumekuwapo na mipango ya kuwahamisha wakazi waishio kwenye hifadh hiyo.

Mimi ni Florence Majani wa DW.