1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yateleza katika orodha ya Maripota wasiokuwa na Mipaka

30 Januari 2013

Shirika la Maripota wasiokuwa na Mipaka limechapisha ripoti yake kuhusu uhuru wa vyombo vya habari kwa mwaka 2012.Barani Afrika Somalia inatajwa kuwa nchi hatari zaidi kwa waandishi habari.

https://p.dw.com/p/17TxT
Mmojawapo wa wanafunzi akilalamika dhidi ya ukosefu wa uhuru wa vyombo vya habariPicha: picture-alliance/dpa

Ripoti ya Maripota wasiokuwa na mipaka inaitaja Somalia kama mahala hatari kabisa kwa waandishi habari mnamo mwaka 2012 : waandishi habari 18 waliouliwa nchini humo,naiwe kwa kujikuta mahala mabomu yalikokuwa yanaripuliwa au kwa kulengwa makusudi na wauwaji .Taifa hilo la pembe ya Afrika limeorodheshwa nafasi ya pili ya nchi hatari kwa waandishi habari baada ya Syria.Nchini Eritrea,inayoburura mkia pia katika orodha hiyo kwa mwaka wa sita mfululizo,hakuna mwandishi habari aliyeuliwa lakini kuna baadhi walioachwa jela hadi kufa.Kuna waandishi habari wasiopungua 30 korokoroni nchini humo hali inayoifanya nchi hiyo iangaliwe kama jela kubwa kabisa ya waandishi habari barani Afrika.Kati ya wafungwa 11 wanaoshikiliwa jela tangu mwaka 2001,sabaa wameshafariki dunia kutoana na hali mbaya katika jela hizo au kwa kujiuwa wenyewe.

Afrika Mashariki pia inaangaliwa kama eneo la mchujo wa habari na kuandamwa waandishi habari.Sudan ya Omar al Bashir ambako magazeti yanazidi kufungwa na kamata kamata ya waandishi habari kuendelea msimu wa kiangazi,inashikilia nafasi ya 170 mkiani,huku Djibuti ambayo pia haina vyombo huru vya habari na inayomshikilia ripota wa kituo cha matangazo cha La Voix de Djibuti,ikikamata nafasi ya 167.Licha ya kuachiwa huru waandishi habari wawwili wa kutoka Sweden,Ethiopia inakamata nafasi ya 137 kutokana na sheria zake za ukandamizaji zilizopitishwa mwaka 2009 na kwasababu ya kuendelea kuwashikilia kizuwizini baadhi ya waandishi habari wa kienyeji.

Tanzania imeangukia nafasi ya 70

Christian Mihr Reporter ohne Grenzen
Christian Mihr , mwenyekiti wa shirika la Maripota wasiokuwa na mipaka nchini UjerumaniPicha: ROG/Günther

Christoph Dreyer wa shirika la Maripota wasiokuwa na mipaka kutoka Berlin anachambua hali ya mambo akisema:"Afrika mashariki hali ni tofauti.Maendeleo mabaya yameripotiwa Tanzania nchi ambayo hadi sasa ilikuwa ikisifiwa sana.Lakini katika mwaka 2012 imepoteza nafasi 36 na kuteleza hadi nafasi ya 70 kutokana na vifo viwili vya waandishi habari.Mmoja alikutikana amekufa,yadhihirika ameuliwa na mwengine ameuwawa wakati wa maandamano.Hii si hali nzuri kwa vyombo vya habari."

Wimbi la mageuzi halikuzisaidia sana nchi za kiarabu

Reporter ohne Grenzen Logo
Nembo ya Maripota wasiokuwa na Mipaka-tawi la Ujerumani

Miaka miwili baada ya wimbi la mageuzi katika nchi za kiarabu uhuru wa vyombo vya habari bado ni tete katika nchi nyingi ikiwa ni pamoja na Misri ambako waandishi habari na wanablogi bado waaendelea kuhujumuiwa ,kukamatwa na kufikishwa mahakamani.Nchini Tunisia waandishi habari wanazidi kushambuliwa na serikali inakawia kutia njiani sheria mpya kuhusu vyombo vya habari.Libya baada ya kung'olewa madarakani utawala wa muammar Gaddafi inaonyekana kufanya vyema na kuchupa nafasi 23 hadi kuifikia nafasi ya 131.

Miongoni mwa nchi za Ulaya, Ujerumani inashikilia nafasi ya 17: Tatizo hapa linatokana na ukosefu wa fedha uliosababisha baaadhi ya vyombo vya habari kufungwa.Sababu nyengine inatokana na ile hali kwamba wajasiria mali uwekeza katika vyombo vya habari ili kuweza kuwa na usemi katika kile kinachoandikwa.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/reporter hne grenzen.de

Mhariri:Yusuf Saumu